Saturday, August 2, 2014

SERENGETI BOYS YAPIGWA 4-0 NA AMAJIMBOS KAMA IMESIMAMA VILE!.




TIMU ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys imebugizwa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Taifa ya vijana wa umri huo ya Afrika kusini maarufu kama Amajimbos katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za vijana za mataifa ya Afrika.

Mechi hiyo rahisi kwa Afrika kusini imepigwa jioni ya leo katika uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto na kushuhudia wenyeji wakitoka na furaha.
Taarifa kutoka nchini Afrika kusini zineeleza kuwa vijana wa Serengeti walizidiwa kila idara na wangepigwa hata mabao 7 kwasababu Amajimbos walikosa nafasi nyingi za wazi.

Serengeti ambao hawakuandaliwa tangu siku nyingi,  wiki mbili zilizopita walitoka suluhu ya bila kufunga katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Licha ya suluhu hiyo, kwa kiasi kikubwa Amajimbos walitawala mchezo huo na kuonekana kuwa vizuri kiufundi na kimbinu.

Mechi ya marudiano mjini Soweto imekuwa nyepesi kwa wenyeji na sasa  Serengeti imetolewa kwa wastani wa mabao 4-0.
Kaka zao Taifa stars wanashuka dimbani kesho kwenye uwanja wa Taifa wa Zimpeto uliopo nje kidogo ya jiji la Maputo dhidi ya wenyeji Msumbiji, kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.

Mechi ya kwanza iliyopigwa wiki mbili zilizopita ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Taifa Stars ilitoka sare ya mabao 2-2 na sasa inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele.

0 Responses to “SERENGETI BOYS YAPIGWA 4-0 NA AMAJIMBOS KAMA IMESIMAMA VILE!.”

Post a Comment

More to Read