Sunday, October 30, 2016
SUMAYE ADAI AMEPATA TAARIFA YA KUTIMULIWA NYUMBANI KWAKE PIA
Do you like this story?
Aliyekuwa
Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye amesema kuwa baada
ya kutangazwa mchakato wa kunyang’anywa shamba lake la Mwabwepande, amepata
taarifa ya kutaka kuondolewa anapoishi pia.
Sumaye
ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kueleza kuhusu kuanza rasmi kwa mchakato wa
kumnyang’anya mwanasiasa huyo shamba la Mwabwepande kwa madai ya kutoliendeleza
kwa muda mrefu.
“Hapa
ninapoishi naambiwa kuna maelekezo yametoka juu kuwa sijapaendeleza. Sasa kama
sijapaendeleza mbona ninaishi hapahapa,” Sumaye amekaririwa na gazeti la Nipashe.
Aidha
Sumaye amesema kuwa ingawa alimsikia Waziri Lukuvi akieleza kuwa tayari
wameshampa notisi ya siku 90 kuhusu kunyang’anywa shamba lake la Mwambwepande,
hadi jana hajaipata notisi hiyo licha ya kufanya jitihada za kuifuatilia.
Alisema
kuwa anashangazwa na uamuzi huo wa Waziri kwani kesi inayolihusu shamba hilo
bado inaendelea mahakamani kutokana na uvamizi wa wananchi na kwamba Mahakama
imezitaka pande zote mbili kutofanya chochote kwenye ardhi hiyo.
Mwanasiasa
huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema alisema kuwa
anachokifahamu ni kwamba alipokea notisi ya kuondolewa katika shamba lake la
Mvomelo kwa madai ya kushindwa kuliendeleza kwa muda mrefu.
“Ninachokijua
ninaandamwa kisiasa. Shamba langu la Mvumelo naambiwa sijaliendeleza. Kwenye
hilo shamba nimejenga nyumba ya kuishi, ghala, kuna trekta na vifaa vingine.
Ninalima mazao na nimefuga zaidi ya ng’ombe 200, nina kondoo 300 na nimechimba
visima viwili vya maji halafu serikali inasema sijaliendeleza,” alisema Sumaye.
Alisisitiza
kuwa ingawa anaamini anaandamwa kisiasa kwa kunyang’anywa mashamba yake,
hatarejea CCM hata akinyang’anywa mashamba yote aliyoanayo.
Sumaye
alihama CCM mwaka jana, miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu na
kujiunga na harakati za kumpigia kampeni mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,
Edward Lowassa. Baada ya uchaguzi huo alitangaza kujiunga rasmi na Chadema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SUMAYE ADAI AMEPATA TAARIFA YA KUTIMULIWA NYUMBANI KWAKE PIA”
Post a Comment