Wednesday, April 9, 2014

RC KANDORO:SHEREHE ZA MAONYESHO NANE NANE ZIMEKOSA UHALISIA.


Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maonyesho ya nanenane ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw Abbas Kandoro akifungua kikao


Wajumbe mbalimbali kutoka kanda za nyanda za juu kusini wakiwa wanamsikiliza kwa makini mwenyekiti


Baadhi ya majengo yaliopo kwenye kiwanja cha John Mwakangale nanenane jijini Mbeya.

Maandalizi ya uwanja wa nanenane wa John Mwakangale Jijini Mbeya.



WAJUMBE wa kamati ya sherehe za maonyesho ya wakulima(Nane Nane)Nyanda za Juu Kusini kwa pamoja wamekubaliana kusimamisha tafrija za usiku wakati wa maonyesho hayo ili kuimarisha ushiriki na kuboresha maonyesho hayo.

Tamko hilo limetolewa  leo na  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo kwenye kikao chwa maandalizi ya maonesho na sherehe za wakulima Nane nane 2014 katika uwanja wa John Mwakangale Jijini Mbeya.

Amesema, kumekuwepo na utaratibu wa  kufanyika kwa tafrija za siku za Mikoa  mara kiongozi anapomaliza kutembelea na kisha  kufanya tathimini  ya shughuli nzima  jambo ambalo limetajwa kuchangia  washiriki kutoelewa maana halisi ya sherehe hizo.

“Sioni umuhimu wa kufanyika kwa tafrija husika kwani washiriki wamekuwa wakinywa pombe na kula nyama ovyo na kuondoa maana halisi ya sherehe za wakulima,”amesema Kandoro.

Aidha, wakiunga mkono tamko hilo baadhi ya wajumbe, wamesema kuwa uchunguzi  umeonesha kwamba maandalizi na ushiriki wa tafrija za usiku yanaathiri utekelezaji wa shughuli za msingi pamoja na kutumia fedha na rasilimali watu.

Hata hivyo mwenyekiti huyo, amesema viongozi wa kiserikali wataendelea na utaratibu wao wa kukagua na kutembelea mabanda ya maonyesho kama kawaida kilichosimamishwa ni tafrija za usiku.

Maonyesho ya Nane Nane Nyanda za Juu kusini inayowakilisha mikoa ya Rukwa, Katavi, Njombe, Iringa, Ruvuma na Mbeya yanatarajia kufanyika Agosti Mosi mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

0 Responses to “RC KANDORO:SHEREHE ZA MAONYESHO NANE NANE ZIMEKOSA UHALISIA.”

Post a Comment

More to Read