Tuesday, April 15, 2014
TEMBO WA HIFADHI YA RUAHA KUFUNGIWA VIFAA MAALUM VYA KUWALINDA DHIDI YA UJANGILI.
Do you like this story?
Viongozi wa makundi ya tembo kati ya 20
na 30 waiishio kwenye ikolojia ya Ruaha wanatarajiwa kufungwa vifaa maalumu kwa
ajili ya kufuatilia nyendo zao ikiwa ni mkakati wa kuwalinda dhidi ya ujangili.
Ikolojia ya Ruaha inayojumuisha Hifadhi
ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) ndio yenye tembo wengi kuliko eneo jingine kwa
Tanzania kwa sasa hivyo zinahitajika juhudi za pamoja katika kuwalinda tembo
hao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu
wa Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa
Tanzania (SPANEST), Godwel Ole Meing'aki alisema eneo hilo lina tembo
wanaofikia 20,090 ambao ni wengine kuliko eneo jingine.
Mpango huo utakaotumia teknolojia ya
kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na
kompyuta utatekelezwa kupitia SPANEST ikiwa ni mkakati wa kuimarisha ulinzi
dhidi ya majangili.
"Kwa kawaida tembo huongozwa na
jike mkubwa ambaye anajua njia na kuelekeza kundi zima na ndio watakaofungwa
vifaa hivyo. Zoezi hili linahitaji gharama kubwa kwa kuwa litahusisha wataalamu
wengi" alisema.
Alisema awali Selous ndio iliyokuwa
ikiongoza kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo hapo awali lakini kutokana na
zoezi la kuhesabu lililofanyika mwaka jana kwa ufadhili wa mradi huo imebainika
kuwa Ruaha inaongoza.
"Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti
wa Wanyama Tanzania (TAWIRI) ambao waliendesha zoezi la kujua idadi ya tembo
eneo la Ruaha ni tembo 20,090 waliopo idadi ambayo huenda miaka michache
iliyopita ilikuwa zaidi ya 30,000", alisema.
Alisema tembo hao watafungwa 'Color'
ambazo zitakuwa na vifaa maalumu vitakavyokuwa vikionesha mahali walipo kwa
nyakati tofauti.
Alisema sambamba na kufanya zoezi hilo
Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) kupitia SPANEST litaimarisha mfumo wa
mawasiliano kwenye hifadhi hizo ili iwe rahisi kwa askari, kituo na kituo
kuweza kuwasiliana kwa urahisi.
Mwenyekiti wa Mpango wa Matumizi Bora
ya Maliasili Idodi na Pawaga (MBOMIPA), unaojumuisha vijiji vyote
vinavyozunguka RUNAPA, Philip Mkumbata alisema mpango huo ni mzuri na utasaidia
kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili hasa dhidi ya tembo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TEMBO WA HIFADHI YA RUAHA KUFUNGIWA VIFAA MAALUM VYA KUWALINDA DHIDI YA UJANGILI.”
Post a Comment