Thursday, June 19, 2014

MICHAEL WAMBURA KIKAANGONI TENA KWA WAKILI LUGAZIYA.




KWA mara ya pili kamati ya Rufani ya uchaguzi ya TFF inakutana leo mchana kujadili rufaa iliyokatwa na mgombea wa Urais katika uchaguzi wa Simba sc, Michael Richard Wambura akipinga kuenguliwa tena katika kinyang`anyiro hicho.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Julius Mutabazi Lugaziya amesema rufaa hiyo ipo mezani na majira ya saa 8 mchana watakaa na kuijadili, huku akiweka wazi kuwa haki itatendeka kwa mrufani.

Mwishoni mwa wiki, Rais wa shirikisho la soka Tanzania, TFF, Jamal Emil Malinzi alitangaza kusimamisha uchaguzi wa Simba akiitaka kamati ya utendaji kuunda kamati ya maadili ili kusikiliza kesi zote za maadili zinazoigubika klabu hiyo.

Igizo la Malinzi lilipingwa na kamati ya uchaguzi ya Simba kwa kueleza kuwa hana mamlaka kikatiba kusimamisha uchaguzi , hivyo uchaguzi uko pale pale yaani juni 29.

Hata hivyo, Rais wa Simba sc, Ismail Aden Rage akiwa mjini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya habari Maelezo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa amezunguza na Rais Malinzi akimuomba uchaguzi ufanyike juni 29 ili kuinusuru klabu hiyo.

Rage alifafanua kuwa kamati ya maadili anayoagiza Malinzi iundwe na kamati ya utendaji haitatenda haki kwasababu robo tatu ya wajumbe ni watuhumiwa wa maadili.
Kujitafutia majaji wa kuwahukumu wao wenyewe haki haitatendeka, hivyo akamuomba Malinzi masuala hayo yarudhishwe kamati za TFF.

Kwa mujibu wa maelezo ya Rage, tayari Malinzi alisharidhia maombi hayo na kumtaka aandike barua ambayo tayari Rage alishapeleka na kwasababu hiyo kamati ya Rufani imepata nguvu ya kuijadili rufani ya Wambura.

Awali kamati ya maadili ya TFF ilitakiwa kukutana wiki iliyopita kujadili malalamiko ya wanachama wa Simba kuhusu baadhi ya wagombea kwenda kinyume na maadili kikatiba hasa wakati huu wa uchaguzi, lakini kutokana na agizo la Malinzi haikuwezekana tena.

Wakili Lugaziya amesema kutokana na maelewano ya Rage na Malinzi kuna uwezekano uchaguzi utafanyika juni 29 na ndio maana wanakutana kujadili rufani ya Wambura.

“Rufani imekuja, nikawaambia wenzangu nina muda leo saa 8, hivyo tutakaa muda huo kujadili”. Alisema Wakili Lugaziya.

“Kama Wambura ana haki atapata, mara ya kwanza sikumbeba, alikuwa na haki akapewa. Na sasa tutaangalia, kama atakuwa na haki atapata, kama atakuwa hana atakosa”. Aliongeza Wakili Lugaziya.
Wambura alienguliwa mara ya kwanza na kamati ya uchaguzi ya klabu ya Simba chini ya mwenyekiti wake, wakili Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kwasababu kubwa mbili ambazo ni kuipeleka Simba mahakamani na kusimamishwa uanachama.

Lakini Wambura alikata rufaa akipinga maamuzi hayo na kamati ya rufani ikamrudisha katika uchaguzi kwasababu Simba walimuacha akifanya shughuli za klabu kama mwanachama hai ikiwemo kulipa ada baada ya kutangaza kumsimamisha mwaka 2010.

Hata hivyo kamati ya Simba ililazimika kumuengua tena kwa madai kuwa Wambura alizungumza maneno yanayoenekana ni kampeni baada ya kurudishwa na wakili Lugaziya.

0 Responses to “MICHAEL WAMBURA KIKAANGONI TENA KWA WAKILI LUGAZIYA.”

Post a Comment

More to Read