Monday, June 16, 2014
RAIS KIKWETE AAGIZA WALIOLIPUA BOMU ZANZIBARA WASAKWE NA KUKAMATWA HARAKA IWEZEKANAVYO
Do you like this story?
RAIS
Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya haki watu wote waliohusika katika ulipuaji bomu lililosababisha kifo
na kujeruhi watu saba mjini Unguja, Zanzibar.
Rais
Kikwete ambaye amesema kitendo hicho ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu
wote wapenda amani Bara na Visiwani, amekitaja kuwa ni cha woga kisicho na
ustaarabu, kisichokubalika katika dunia ya sasa.
Alisema
hayo katika salamu za rambirambi alizotuma jana kwa Rais Ali Mohamed Shein wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Bomu hilo
lilirushwa katika shughuli ya kidini iliyokuwa ikifanyika katika eneo la
Darajani , mjini Unguja. Miongoni mwa majeruhi, yumo mhubiri wa amani
ajulikanaye kama Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa Zanzibar.
“Hicho
ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na
Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala hakikubaliki
katika dunia ya sasa,” alisema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Hiki
ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu wa aina yeyote ile.”
Alikemea
wanaofanya vitendo hivyo na akahimiza watu kuwa wastaarabu, wavumilivu na
kuheshimu imani na mitizamo ya watu wengine hata kama hawakubaliani nao.
Akiendelea
kulaani, alisema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na ustaarabu ambao
wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini ambapo ndipo
mahali panapostahili amani, uvumilivu na unyenyekevu zaidi kwa kuwa ni wakati
ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na muumba wake.
Alihimiza
polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki wahusika wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa Zanzibar,
Yussfu Ilembo, aliyekufa papo hapo ni Muhammad Mkombalaguha (26), mkazi wa
Tanga.
Kutokana
na tukio hilo, polisi visiwani humo ilitangazia hali ya hatari kwa watu
waliohusika na shambulio hilo. Ilielezwa kwamba uchunguzi umeanzia kwenye
mabaki ya vitu vilivyokutwa katika eneo la tukio.
Miongoni
mwa vielelezo vilivyokusanywa ni pamoja na vipande vya mabaki ya gundi ya
karatasi na vitu vingine ambavyo vinasadikikwa vimetumika kutengeneza bomu
hilo.
Mtu
aliyekufa pamoja na majeruhi, walikutwa na mkasa huo wakati wakitoa Msikiti wa
Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia saa 1:45 usiku na
kuendelea.
Baada ya
kumalizika ibada hiyo, walitoka msikitini na kufika eneo la Darajani wakisubiri
gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao unasadikiwa kuwa ni bomu.
Katika
hatua nyingine, akiwa mkoani Dodoma juzi, Rais Kikwete aliwataka Watanzania
kuendelea kulinda na kupigania amani iliyopo kwa ustawi na usalama wa nchi .
Rais
Kikwete alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa tamasha la uzalendo lililoasisiwa
na wasanii wa muziki na filamu nchini ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa video ya
wimbo maalumu wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema
uzalendo kwa Watanzania ndiyo njia pekee ya kufanya taifa liendelee kutunukiwa
hadhi ya kisiwa cha amani duniani.
Katika tamasha
hilo lililofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema ili
kuwaenzi waasisi wa taifa, ni lazima kudumisha misingi ya amani na kujitolea
kizalendo kulilinda na kulitetea taifa kama walivyofanya waasisi Mwalimu Julius
Nyerere na Shehe Abeid Amani Karume.
Pia
aliwataka wasanii kutumia vizuri talanta walizojaliwa kufikisha ujumbe wenye
uzalendo kwa Tanzania.
Credit: Habari Leo
Credit: Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS KIKWETE AAGIZA WALIOLIPUA BOMU ZANZIBARA WASAKWE NA KUKAMATWA HARAKA IWEZEKANAVYO ”
Post a Comment