Tuesday, July 8, 2014

WAKUFUNZI 33 WAPATIWA MAFUNZO MKOANI IRINGA.



Na Friday Simbaya,
Jumla ya wakufunzi 33 kutoka wilaya za Mufindi na Iringa Vijini wapatiwa mafunzo ya ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (misitu na wanyamapori) katika mafunzo ya siku tisa yaliofanyika mjini Iringa katika Ukumbi VETA, kuanzia tarehe 25/06 hadi 03/07 mwaka huu.

Mafunzo hayo yalishirikisha asasi nne ambapo kwa wilaya ya Mufindi ni ASHTECH na MUVIMA na kwa Iringa vijijini ni MJUMIKK na MBOMIPA pamoja na washiriki wengine 17 kutoka kata ambao nao watashiriki kutoa mafunzo ya mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili, kama vilevile
maafisa tarafa, madiwani na maafisa maendeleo ya jamii, na Watendaji wa kata.

Meneja wa mradi huo, Dkt. Naima Besta alisema mafunzo hayo yameganyika katika sehemu nne ambapo mafunzo ya awali yawakufunzi yalitolewa kwa timu ya mradi kutoka LEAT; mafunzo ya pili ni kwa wakufunzi 33 kutoka wilaya ya Mufundi na Iringa vijini, mafunzo ya watendaji wanaohusika na maliasili katika ngazi ya wilaya ambayo yatafuatiwa na mafunzo ya wanakamati mbalimbali za maliasili katika ngazi ya vijiji na sehemu ya mwisho ni mafunzo kwa wananchi wote katika vijiji 14 vilivyoko Mufindi na Iringa vijijini.

Alisema kuwa mafunzo kwa ngazi ya wilaya yatawahusisha maafisa wanyamapori, maafisa ardhi, maafisa misitu pamoja na kamati mbalimbali za mazingira.
"Huu ni mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili
unakusudia kuwawezesha wananchi kushiriki katika kuisimamia serikali kutimiza wajibu wake katika kusimamia maliasili kwa kuwapatia elimu, nyenzo na mbinu zifaazoza kuwajibisha asasi za serikali zenye dhamana ya
usimamizi wa maliasili.

Mafunzo hayo ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii ambao yanawalenga wananchi kujua kuwa ni haki yao kupata ufafanuzi, uthibitisho na uhalalisho (3Us) juu ya namna ambavyo rasilimali za umma zinavyosimamiwa na jinsi ambavyo rasilimali hizi hasa zinazotokana na maliasili zinaendelea na zitaendelea kuhakikisha upatikanaji na ulindwaji wa haki za msingi za binadamu. Lengo kuu nikuongeza ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili," alisema meneja wa mradi.

Naye mshiriki kutoka Asasi ya Mbomipa Idodi na Pawaga wilayani Iringa, mwalimu Ngoola Mwangosi alishukuru shirika la LEAT kwa kuwapatia mafunzo hayo ambapo alisema kuwa yamekuja wakati mwafaka ambapo maeneo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inakabiliwa na tatizo la ujangili wa tembo kwa sababu yatasaidia kupunguza vitendo katika maeneo ya hifadhi.

"Mafunzo haya yametujengea uwezo wa kufahamu mwelekeo sahihi wa uwajibikahi jamii katika usimamizi wa maliasili (misitu na wanyamapori)," alisema mwalimu Mwangosi.
Alisema kuwa mafunzo ya ufuatilaji wa uwajibikaji jamii yamewajengea uwezo wa kutambua sheria na sera mbalimbali zinazosimamia misitu na wanyamapori.

Mshiriki mwingine Gertrude Mkongwa kutoka shirika la MUVIMA wilayani Mufindi alisema mafunzo hayo yamemsaidia kutoka hatua moja hadi nyingine kwa sababu hakuwa na uelewa wowote kuhusu sheria na sera mazingira, misitu na wanayamapori na maliasili kwa ujumla.
Mkongwa alisema kuwa mafunzo hayo yamemuogeza uelewa juu ya zana za uwajibikaji na usimamizi jamii kwa kufuatilia kila hatua ya mchakato.

Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili unatekelezwa na Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Maendeleo ya Kimataifa
la Marekani (USAID) kutoka kwa Watu wa Marekani.

Hivyo basi, LEAT ni asasi isiyokuwa ya kiserikali inayofanya shughuli za ulinzi na usimamizi wa mazingira na rasilimali nyingine kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na: Kuleta na kukuza utawala bora wa usimamizi na ulinzi endelevu wa mazingira na maliasili kwa kufungua na kuendesha kesi mahakamani zenye kupigania usimamizi na ulinzi mzuri wa mazingiran na rasimali zake kwa masilahi ya watu na jamii.

Kufanya ushawishi na utetezi wa mazingira na rasilimali zake, kufanya tafiti-mkakati zenye lengo la kuchagiza usimamizi na ulinzi wa mazingira na rasilimali zake, kuwajengea uwezo wananchi na kufanyakazi nao kwa pamoja na kimtandao, Kuwajibisha taasisi za serikali zenye dhamana ya usimamizi mazingira na rasilimali zake,

Kupigania utunzaji na usimamizi mzuri wa mazingira na rasilimali zake pamoja na ardhi na kupigania kuheshimiwa na kufuatwa kwa ukamilifu sheria zote zinazohusika na usimamizi na ulinzi wa mazingira, maliasili.

LEAT kwa kushirikiana na USAID inatekeleza mradi huu wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi na ufuatiliaji wa maliasili ili kuboresha uwajibikaji wa serikali, taasisi na idara zake zenye dhamana ya usimamizi wa maliasili ili kuwezesha usimamizi mzuri wa mazingira na maliasili, mgawanyo wa haki wa faida na manufaa yatokanayo na maliasli, utawala bora na utoaji wa huduma nzuri kwa jamii katika ngazi za wilaya, kata na vijiji katika wilaya ambapo mradi huu unatekelezwa.

0 Responses to “WAKUFUNZI 33 WAPATIWA MAFUNZO MKOANI IRINGA.”

Post a Comment

More to Read