Tuesday, July 22, 2014

WANASHERIA WAHOJI UHALALI WA BUNGE LA KATIBA BILA UKAWA?




Zikiwa zimebaki wiki mbili kuanza vikao vyake, baadhi ya wanasheria wamehoji uhalali wa Bunge hilo kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba bila ya kuwapo kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Wamesema msimamo wa Ukawa kukataa kurejea katika vikao vya Bunge hilo na kushikilia msimamo wa kutaka ijadiliwe Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, utafanya akidi ya wajumbe kwa ajili ya kupitisha uamuzi katika Bunge hilo kutotimia.
Wanasheria hao waliohojiwa jana kuhusu msimamo wa Ukawa kususia Bunge na hatima ya Katiba Mpya wamesema hakuna uwezekano wa kisheria kuipitisha wala kufanya mabadiliko ya vifungu ili kupata uhalali wa kufanya hivyo.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Julai 8 mwaka huu, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alisema iwapo Ukawa watarudi bungeni lakini wakasusa tena kadri mjadala utakavyoendelea, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.

Hata hivyo, wanasheria hao walisema kwamba bila kuwapo maridhiano, Bunge hilo haliwezi kufikia tamati na si rahisi kupata akidi ambayo si tu inatakiwa na Kanuni za Bunge na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bali pia Katiba ya sasa.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Kifungu cha 26(2) kinaeleza: “Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Zanzibar.”

Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jesse James alisema iwapo hakutakuwa na maridhiano hakuna chochote kinachoweza kufanyika au kupitishwa zaidi ya kuahirisha Bunge hilo hadi pale watakapokubaliana.

0 Responses to “WANASHERIA WAHOJI UHALALI WA BUNGE LA KATIBA BILA UKAWA?”

Post a Comment

More to Read