Monday, August 18, 2014

JUMA MWAMBUSI SASA AANZA MAJIGAMBO KUELEKEA LIGI KUU BARA.





SIKU chache baada ya timu yake kuanza ziara katika mikoa jirani na Mbeya, Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi ametamba timu yake itafanya maajabu ambayo yatashangaza wadau wengi wa soka nchini tofauti na msimu uliopita.

Mwambusi alisema ana mbinu mpya kabisa atakazozitumia kwa vijana wake huku akiwataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutegemea mambo makubwa msimu ujao.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo juzi Jumamosi mjini Sumbawanga alipokuwa akizungumzia malengo na mikakati yake ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara wakati timu hiyo ikifanya ziara ya kuwatembelea mashabiki na wapenzi wake mikoa ya Rukwa na Katavi ikiwa ni maandalizi ya kuingia rasmi kambini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema: “Mipango yangu ni kuiona Mbeya City inatwaa ubingwa, msimu uliopita tulikuwa na hofu ya ugeni kwenye ligi hiyo lakini tulifanya vizuri. Msimu huu Mbeya City inakuja kivingine kabisa wapenzi na mashabiki wetu wategemee mambo makubwa msimu ujao.
“Baada ya kupata mialiko kutoka kwa mashabiki wetu walioko Rukwa na Katavi ya kuwatembelea nimeona ni fursa nzuri ya kucheza mechi za kirafiki na wenyeji ili kuweza kuangalia kasoro zilizopo kwa wachezaji wangu kwani wametoka mapumzikoni.”

Katika msimu uliopita Mbeya City iliyoshiriki ligi kuu kwa mara ya kwanza, ilimaliza katika nafasi ya tatu huku ikitoa changamoto kubwa kwa timu zilizoshiriki ligi hiyo.
Chanzo:Mwanaspoti

0 Responses to “JUMA MWAMBUSI SASA AANZA MAJIGAMBO KUELEKEA LIGI KUU BARA.”

Post a Comment

More to Read