Monday, August 18, 2014
PHIRI AONGEZA DOZI MSIMBAZI, HANS POPPE ASAKA VIFAA KIGALI, YANGA, COASTAL HAOOO! PEMBA.
Do you like this story?
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wanaendelea
vyema na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia
kuanza kushika kasi septemba 30 mwaka huu.
Simba wamepiga kambi visiwani Zanzibar
(Unguja) chini ya kocha mkuu mpya, Mzambia, Patrick Phiri akisaidiwa na kocha
msaidizi, kiungo wa zamani wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa
Stars’, Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ na kocha wa makipa, Idd Pazzi
‘Father’.
Simba ilianza programu ya mazoezi mara
moja kwa siku hapo jana katika fukwe za bahari ya Hindi, lakini Phiri ameamua
kuongeza dozi ambapo leo atafanya mazoezi mara mbili, (asubuhi na jioni).
Lengo la Phiri ni kupata muda wa
kutosha wa kusuka kikosi chake akijua wazi kuwa msimu ujao atakumbana na
changamoto kubwa ya kusaka ubingwa wa Tanzania bara.
Pia kocha huyo alisisitiza suala la
mechi za kirafiki ili kukiona kikosi chake kwa mara ya kwanza na kujua nini cha
kufanya zaidi.
Kocha huyo aliyerejea nchini kwa mara
ya tatu kuifundisha Simba baada ya kutimuliwa kwa Mcroatia, Zdravko Logarusic
‘Loga’ aliahidi mambo mazuri kwa Simba iliyoshinda kuwika kwa miaka mitatu
mfululizo.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa kamati ya
usajili ya Simba, Keptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
Zacharia Hans Poppe yuko mjini Kigali, nchini Rwanda kufuatilia michuano ya
kombe la Kagame inayoendelea nchini humo.
Uwepo wa Poppe huko Kigali unatafsiriwa
kuwa ni kujaribu kuona vifaa vipya vya kuongeza Msimbazi ikizingatiwa
Shirikisho la soka Tanzania jana limetangaza kuongeza siku 10 zaidi za usajili
mpaka Agosti 27 mwaka huu badala ya siku ya mwisho iliyokuwa jana Agosti 17.
Katika siku hizo zilizoongezwa mtu
makini na mwenye mapenzi makubwa na Simba sc, Hans Poppe anaweza kuibuka na
vifaa vipya hususani wakati huu Kombe la Kagame likifikia hatua ya robo fainali
itakayoanza kutimua vumbi leo hii.
Wakati hayo yakijiri Msimbazi, nao
mahasimu wao, Dar Young Africans wanatarajia kuondoka wiki hii jijini Dar es
salaam kuelekea kisiwani Pemba, Zanzibar ambapo wataweka kambi ya kujiandaa na
ligi kuu Bara.
Yanga sc watakuwa huko chini ya kocha
anayesemekana kurudisha morali ya kila mchezaji kwasasa, Mbrazil, Marcio
Maximo.
Nao wagosi wa Kaya, Coastal Union
wanatarajia kutua Pemba kesho jumanne,.
Kwa maana hiyo, mashabiki wa Zanzibar
watashuhudia timu tatu za ligi kuu soka Tanzania bara zikijivua katika ardhi
yao inayosifika kwa uzalishaji wa zao la Karafuu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “PHIRI AONGEZA DOZI MSIMBAZI, HANS POPPE ASAKA VIFAA KIGALI, YANGA, COASTAL HAOOO! PEMBA.”
Post a Comment