Monday, August 25, 2014

SERIKALI YAITAKA TFF KUTUMIA MAKOCHA WAGENI KUNOA MAKOCHA WAZAWA




Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni Juma Nkamia akizungumza wakati akifunga mashindano ya mbio za baiskeli Kanda ya ziwa yaliyoandaliwa na chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) chini ya udhamini wa kampuni ya Uchimbaji madini ya African Barrick Gold (ABG) huku kauli mbiu ikiwa ni “Tufanikiwe pamoja”-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog.




Serikali imemuomba  rais wa shirikisho la  Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamali Malinzi kuweka  utaratibu wa Makocha wa kigeni wanaokuja hapa nchini kuifundisha timu ya taifa  kuwa wanatoa mafunzo ya kitalaamu ya mpira huo kwa makocha wazawa hali ambayo itasaidia pale makocha hao wanapomaliza mikataba  yao  wazawa wawe wamefaidika na utaalamu wa wageni hao.
Ombi hilo lilitolewa juzi  mjini Kahama mkoani Shinyanga na naibu Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni Juma Nkamia wakati akifunga mashindano ya mbio za baiskeli Kanda ya ziwa yaliyoandaliwa na chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) chini ya udhamini wa kampuni ya Uchimbaji madini ya African Barrick Gold (ABG) huku kauli mbiu ikiwa ni “Tufanikiwe pamoja”.
Nkamia alisema endapo chama mpira miguu nchini kitaweka utaratibu italeta faida kwa makocha wazawa kwa kuongezewa ujuzi kupitia mafunzo yatakayokuwa yakitolewa na hivyo kuchangia kwa kiasi fulani kuinua soka la Tanzania ambalo kwa mwaka huu timu zake zote zimefanya vibaya katika mashindano ya kimataifa.
Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa alisema kuwa katika kipindi cha mwaka huu Tanzania imefanya vibaya sana katika mashindano ya kimataifa huku akitolea mfano kutolewa kwa timu ya Azam Fc  katika mashindano ya kombe la Cecafa na pia kufanya vibaya kwa Timu ya Taifa katika mashindano ya kufuzu kucheza kombe la mataifa ya Africa na pia michezo ya Jumuia ya Madola.
Kwa upande wake katibu wa chama cha Baiskeli  nchini John Machemba alisema mashindano ya mbio za baiskeli Kanda ya ziwa yalikutanisha washiriki kutoka mikoa sita ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Geita ,Mara na wenyeji Kahama(mkoa maalum).
Alisema katika mashindano hayo washiriki wakiwa ni kike na kiume ambapo wanaume walikimbia umbali wa kilometa 156.5 ikiwa ni kutoka eneo la Phantom mjini Kahama,kwenda eneo la Manzese mjini Kahama hadi Tinde  kisha kurudi mjini Kahama wakati wanawake walikimbia umbali wa kilomea 80 kutoka mjini Kahama hadi eneo la Sungamile halmashauri ya mji Kahama.
Kwa upande wake makamu wa  rais wa African Barrick Gold  Deo Mwanyika alisema kampuni yake imetumia jumla ya shilingi milioni 150 katika kuhakikisha kuwa mashindano hayo ya mbio za baiskeli na kuongeza kuwa Barrick inafanya uchimbaji wake huku iwajali majirani zake.
Mwanyika alisema pamoja African Barrick Gold  kujikita katika kusaidia huduma za kijamii kama vile sekta za afya, elimu, maji, na miundombinu lakini kwa sasa nguvu kubwa wameilezekeza katika michezo ikiwa ni sambamba na mbio za baiskeli ili kupata washiriki wazuri watakaowakilisha kanda ya ziwa katika mashindano ya kitaifa huko katika mkoa wa Mbeya mwishoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo Mwanyika alisema  udhamini wao katika mbio za baiskeli ni wa miaka mitatu na kuwataka wadau mbalimbali kutoa ushirikiano kuwa wapi wanakosea au wanapatia kwa lengo la kuboresha.
Katika Masindano hayo mshindi wa kwanza kwa Wanawake alikuwa ni  Martha Anthony Kutoka Mwanza aliyepata kitita cha shiulingi milioni 1.2, mshindi wa pili alikuwa Salome Donald kutoka Shinyanga  aliyeondoka na shilingi 800,000 wakati mshindi wa tatu ni Laurencia Luzuba kutoka Mwanza alipata shilingi 600,000  wote wakipewa vikombe na medali na mshindi wa nne mpaka wa kumi walipata shilingi  250,000 huku wa 11 hadi 20 wakipata shilingi 150,000.
Kwa upande wa wanaume mshindi wa kwanza alikuwa Masunga Duba  kutoka Mwanza aliyetumia Saa 4 dakika 13 na sekunde 58 na  kuondoka na kitita cha shilingi milioni  1.5, Seni Konda kutoka Shinyanga alikuwa mshindi wa pili na  na kupata shilingi milioni moja wakati Simon Mbaruku kutoka Simiyu alikuwa wa tatu na kupata shilingi 700,000,wote hawa walipewa vikombe na medali.
Mshindi wa nne hadi wa kumi walipata  500,000 na wa 11 hadi 20 walipata 250,000 huku 21 hadi 30 wakipata shilingi 150,000.

Na Kadama Malunde-Kahama

0 Responses to “ SERIKALI YAITAKA TFF KUTUMIA MAKOCHA WAGENI KUNOA MAKOCHA WAZAWA”

Post a Comment

More to Read