Wednesday, August 13, 2014

WANAWAKE WAYAZUIA MAGARI YA JESHI KUPINGA WAUME ZAO KUPELEKWA KUPAMBANA NA BOKO HARAM.



Ripoti kutoka Nigeria zinaeleza kuwa Jumamosi iliyopita kundi kubwa la wanawake lilijitokeza na kuzuia magari ya jeshi yaliyokuwa yamewabeba wanaume wao na wake zao yakielekea katika mji wa Gwosa, sehemu ambayo inadhibitiwa na kundi la Boko Haram.

Kwa mujibu wa Prime Times ya Nigeria, wanawake hao walizua geti la barracks katika mji wa Borno huku wengine wakilala barabarani kushinikiza waume zao wapewe vifaa vya kisasa na imara zaidi ndipo waende vitani kupambana na kundi hilo.

Hali hiyo imekuja baada ya kuripotiwa kuwa karibu wanajeshi 60 waliuawa Jumatano iliyopita katika eneo la Gwosa linalomilikiwa na Boko Haram na kudaiwa kuwa sababu kubwa ni zana duni walizokuwa nazo kulinganisha na zana za kisasa za kijeshi za kundi hilo.

Chanzo kimeiambia Prime Times kuwa wanawake hao walieleza kuwa hawataki kubaki wajane na yatima kama wenzao kwa sababu ya vita hiyo.

“Mwanamke mmoja alisema ‘hatutaki kuwa kundi lingine la wajane, wapeni waume zetu zana bora zaidi za kivita, silaha na magari bora zaidi la sivyo hawaendi kokote’.”

Wanajeshi wengine pia walionekana kuunga mkono madai ya wanawake hao na kusukuma lawama kwa maafisa wa serikali.


Kundi la Boko Haram bado linawashikilia mateka wanafunzi wa kike zaidi ya 200 na wanawake wengine huku likitekeleza mauaji ya kutisha katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.



0 Responses to “WANAWAKE WAYAZUIA MAGARI YA JESHI KUPINGA WAUME ZAO KUPELEKWA KUPAMBANA NA BOKO HARAM.”

Post a Comment

More to Read