Wednesday, November 11, 2015

CCM LUDEWA YAMPITISHA NGALAWA KUWANIA UBUNGE




SIKU ya jana haikuwa nzuri kwa baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya marehemu Deo Filikunjombe baada ya mdogo wake Phillip Filikunjombe kushika nafasi ya pili katika kura za maoni ya ubunge wa jimbo la Ludewa zilizofanyika jana, mjini Ludewa.

Uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo uliahirishwa baada ya aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, Deo Filikunjombe kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Oktoba 15, siku 10 kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu.

Phillip Filikunjombe aliyekuwa anategemewa na wengi kushinda kura za maoni za jimbo hilo ili aingie moja kwa moja katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo lililoongozwa na kaka yake Deo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, amepata kura 501 akizidiwa na Deo Ngalawa aliyepata kura 537.

Filikunjombe aliangushwa na mgombea mwenzake huyo katika kinyang’anyiro kilichoshikilisha wagombea saba, baada ya wengine watatu kujitoa kwa ombi la kumuunga mkono Filikunjombe.

Waliojitoa katika kinyang’anyiro hicho kilichomshilikisha msanii wa vichekesho na muimbaji wa nyimbo za injili, Emmanuel Mgaya maarufu kwa jina la ‘Masanja Mkandamizaji’ aliyeambulia kura 19 ni pamoja Johnson Mgimba na Simon Ngatunga.

Wengine walioshiriki kura hizo za maoni na kura zao kwenye mabano ni James Mgaya (72), Dk Evaristo Mtitu (21) na Zephania Chaula (21) na Mpangala Mpangala (3).

0 Responses to “CCM LUDEWA YAMPITISHA NGALAWA KUWANIA UBUNGE”

Post a Comment

More to Read