Saturday, February 25, 2017
WAZIRI MWIJAGE AWAONYA WAWEKEZAJI
Do you like this story?
Waziri wa biashara, Viwanda na
Uwekezaji, Charles Mwijage, amezitaka taasisi zinazohusika na uwekezaji
kutokuwa na ukiritimba ili hali kufikia malengo ya serikali ya kukuza
sekta ya viwanda.
Aidha ameeleza kwamba, wizara hiyo, imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yatawezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Hayo aliyasema huko kitongoji cha Pingo
Chalinze,Bagamoyo,wakati akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha
Vigae cha Twyford Ceramics Ltd.
Mwijage alisema, uwekezaji huo unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda .
Alisema kwa kuanzishwa viwanda vingi vya aina hiyo kutasaidia kuongeza pato la nchi na kuzalisha ajira kwa wingi.
“Zipo idara ambazo zinafanikisha
uwekezaji ikiwemo brela, idara ya uhamiaji, kazi, mamlaka ya mapato TRA,
wizara ya ardhi, shirika la viwango TBS, baraza la Mazingira NEMC
ambazo zinapaswa kufanya kazi kwa wepesi ili kufanikisha uwekezaji,”
alisema Mwijage.
Alisema kati ya idara hizo baadhi zimekuwa zikifanya vizuri lakini nyingine zimekuwa zikiwapa usumbufu mkubwa wawekezaji.
“Wizara yangu haina tatizo lakini
kuna baadhi ya idara zimekuwa kero na ukiritimba usio na sababu .,naomba
kama kuna idara zinakuwa kikwazo niambieni ili tuwachukulie hatua,” alisema Mwijage.
Mwijage alisema nchi zilizofanikiwa
kukuza uchumi wake kupitia viwanda zimeweza kutoa ajira nyingi kwa
vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi.
Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho Jack
Feng alieleza, kiwanda hicho asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka
nchini ambapo kigae kinatumia maliahafi zaidi ya 10.
Alisema mara kiwanda hicho
kitakapokamilika agosti mwaka huu kitaweza kupunguza asilimia 30 ya
uagizaji wa vigae toka nje ya nchi.
Feng alisema wanatarajia kuajiri
wafanyakazi 2,000 moja kwa moja na 4,000 kazi za muda na gharama ya
mradi huo ni dola mil. 56 sawa na bil. 120 .
Alisema watauuza hadi nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi .
Nae mkurugenzi mtendaji wa kituo cha
uwekezaji Cliford Tandari alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni wa
mfano kwani utavutia makampuni mengi.
Alisema kwasasa kituo hicho kimeweza
kutoa wigo mkubwa katika kuandikisha miradi mbalimbali toka china na
kufikia miradi 667 ambayo itazalisha ajira 83,141 kwa watanzania ,miradi
452 ni miradi inayohusiana na sekta ya uzalishaji viwandani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema ,mkoa huo una viwanda 264 huku vikubwa vikiwa ni viwili.
Ndikilo alisema uwekezaji huo ni mkubwa na unatarajia kukuza ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Alisema mkoa wa Pwani bado una maeneo
makubwa ya uwekezaji na tayari kuna eneo lenye ukubwa wa hekari 5,000
linahitaji wawekezaji .
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete aliwapongeza wawekezaji hao kutoka nchi ya China, alisema Chalinze imejipanga kuwa sehemu ya uwekezaji ambapo kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto kubwa inayokabiliwa wananchi na wawekezaji ni ukosefu wa maji.
Alibainisha wamekuwa wakijitahidi
kuikabili lakini bado hawajafanikiwa kuidhibiti aliomba wawekezaji hao
kutoa ajira bila ya kuwabagua wenyeji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MWIJAGE AWAONYA WAWEKEZAJI”
Post a Comment