Friday, April 28, 2017

BAADA YA MANARA, KADI TATU ZA FAKHI ZATUA KWA MJUMBE WA YANGA




Bodi ya ligi Tanzania imemfungulia mashitaka, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu ya Yanga, Salum Mkemi, mbele ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Taarifa ya Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura imesema kwamba Mkemi aliishutumu na kuidhalilisha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ijulikanayo kama Kamati ya Saa 72, kupitia vyombo vya Habari kwa kusema inaendeshwa kiunazi na imegubikwa na rushwa.

Wambura amesema Mkemi aliishitumu Kamati ya Saa 72, iliamua suala la kadi tatu za njano za mchezaji Mohammed Fakhi Gharib wa Kagera Sugar kwa upendeleo kutokana na rushwa waliyopewa na Simba SC.

Aidha, Wambura amesema madai ya Mkemi sio ya kweli na yana lengo la kuwakashifu na kuwadhalilisha viongozi wa TFF na Kamati ya Saa 72 mbele ya mashabiki wa mpira miguu na Watanzania kwa ujumla.

“Kutokana na kitendo hicho ambacho kina lengo la kusababisha vurugu kwenye mpira wa miguu, tunaomba mlalamikiwa aadhibiwe kwa mujibu wa ibara ya 53 (1) na (2) ya kanuni za Nidhamu za TFF pamoja na kanuni ya 41 (2) ya Ligi Kuu,”amesema Wambura na kuongeza; “Pia apewe adhabu nyingine kama ambavyo Kamati ya Nidhamu itaona inafaa kwa kuzingatia Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012,”.
BY HAMZA FUMO

0 Responses to “ BAADA YA MANARA, KADI TATU ZA FAKHI ZATUA KWA MJUMBE WA YANGA”

Post a Comment

More to Read