Thursday, July 21, 2016
KINANA ATOA MASHARTI ENDAPO RAIS MAGUFULI ATAMHITAJI AENDELEE KUWA KATIBU MKUU WA CCM
Do you like this story?
KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno endapo Rais
John Magufuli atamhitaji kuendelea na wadhifa huo, huku akibainisha kuwa
amekutana na changamoto nyingi katika nafasi hiyo kiasi kwamba wakati mwingine
alikata tamaa.
Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jeshi.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu wa CCM
utakaofanyika keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa
miaka mitatu na nusu, alisema aliombwa katika nafasi hiyo baada ya kuwa aliamua
kustaafu, lakini akakumbana na changamoto mbalimbali.
CCM
kuwa mbali na wananchi
Alisema
kuna wakati aliona kama vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba
hakikuwa karibu sana nao.
“Ninyi
ni mashahidi, ikabidi kubuni utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili chama
kiwe karibu na wananchi, kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi kifuatilie
matatizo yao kisimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,” alisema Kinana na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo
amekuwa akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili ya matatizo kutatuliwa.
“Changamoto
ya pili ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma kulikuwa
na misukosuko kidogo ya umoja na mshikamano, kushutumiana na kulaumiana,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni
kuimarisha umoja ndani ya chama, kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha
chama kinajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kurejea katika misingi yake ya awali
katika maeneo ya uadilifu, uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi.
Azuiwa
ziarani
Kinana
alisema amekwenda wilaya zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi na
amesafiri zaidi ya kilometa 192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700 ya aina
mbalimbali ya ndani na nje na haikuwa kazi rahisi
“Changamoto
nilizokutana nazo ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati mwingine
kufanya ziara kwenye maeneo fulani fulani niliambiwa ni hatarishi siwezi kwenda
kwa hiyo ilibidi nibishane na viongozi na watendaji wakuu wa serikali…nikasema
hapana nimeamua kwenda lazima niende,”
alisema Kinana.
Katibu
huyo akitoa mfano alisema kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka Nyamisati
wilayani Rufiji kwenda Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani walifikiri si njia
salama ya kusafiri na kumpelekea ujumbe asisafiri kwa boti, bali asafiri kwa
ndege, lakini alisema hapana ataondoka kwa boti.
“Walichofanya
wakakaa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia barua
rasmi kwamba tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa maana
nyingine walikuwa wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile vile
kunitisha kidogo kwamba si salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.
Ashitakiwa
kwa JK
“Baadaye
Rais mstaafu Kikwete alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda
kumwambia tumezungumza na Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia barua ya
kumuomba asisafiri na boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu sana…nikamjibu
rais nakuheshimu mamlaka yako ni makubwa si vizuri nikakukatalia, lakini
niruhusu nikukatalie kwa sababu hata wananchi wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha
maisha yao, ni vizuri na mimi nikahatarisha maisha yangu hata kidogo…
akaniambia nimekuelewa endelea,”
alibainisha.
Alisema
zipo changamoto nyingi sana nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela, mkuu wa
mkoa akamuambia boti haifai kusafiri akasema mara haiwezi kusafiri imeharibika.
“Nikazungumza
na Mwakyembe akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi, lakini
changamoto zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari moja tu ndio
inayoshuka chini hakuna kupishana magari nikaambiwa nisiende nikasema nina
kwenda,” alisema na kuongeza kuwa kulikuwa
na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja kidogo ambaye hasikilizi
ushauri sana.
Pia
nyingine zinazotokana na changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa wakati,
mbolea kutofika kwa wakati, halmashauri kutopata fedha za maendeleo kwa wakati,
watumishi wa umma wanaohamishwa kwenda vijijini hawaendi vijijini kwenda
kuwahudumia wananchi, tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji
kati ya wananchi na hifadhi za taifa.
“Ndio
maana mnaniona siku hizi nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa
nikiyaombea yanafanyika, umangimeza haupo watu wachape kazi wawahudumie
wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa inapigwa vita, uwajibikaji na uadilifu
unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na hayo yasipofanyika mtu anaondolewa mara
moja,” alifafanua Kinana ambaye kuanzia
mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha
chama chake na kuibana serikali.
Kurejea
kwake CCM
“Yalitokea
mazingira ambayo niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama kuniomba
niwe mtendaji mkuu wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda, bali niliitwa
na nikakalishwa wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni wito na kwa kuwa ni
watu ninaowaheshimu na wana dhamana kubwa kwenye nchi yetu, nikakubali kufanya
kazi hiyo,” alisema Kinana akizungumzia jinsi
alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Alisema
amekuwepo katika uongozi ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani ya
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka wa
kung’atuka.
“Mwanasiasa
mzuri ni yule anayejua wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati mzuri
wa kung’atuka kuachia waingie wenye umri wa kati na umri wa vijana kuachia
waongoze chama na kuwaamini,”
alieleza.
Alisema
moja ya mambo ambayo walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha chama,
kusimamia na kumsaidia mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata wagombea
kwenye nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi kuendesha
shughuli za kampeni na uchaguzi na utakamalizika.
“Uchaguzi
umekwisha niruhusiwe kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda umefika
kwa hiyo nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika sasa wengine
wakaniuliza hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee hamjawa wazee kiasi
cha kusahau ndio haya tuliyokubaliana,”
alieleza.
Akiombwa
na JPM
Alipoulizwa
kama akiombwa na Rais Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme
hajasema, hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye kikao kama
akiniomba, tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika kama nilivyokuwa na
mazungumzo na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka 2012.”
Waliokisaliti
chama
Akizungumzia
walioisaliti CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM alisema
msaliti yeyote adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha siasa.
“Kwenye
CCM wapo watu walioyumba, kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu waliyumba
hivi kidogo wakakaa mguu upande huku hawapo na kule hawapo, wako ambao sio tu
waliyumba, bali walikiuka maadili na hawakushiriki kwenye shughuli za kampeni,”
alisema.
Pia
alisema wapo ambao hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani na kila
mtu atakuwa na adhabu yake kulingana na makosa yake.
“Kama
mmekuwa mkifuatilia kuna waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa. Kwa
mfano, Shinyanga 123 walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa kuchukuliwa hatua
kwenye ngazi za juu, sasa jambo moja mtu yeyote kabla ya kuchukuliwa hatua
lazima aelezwe mashtaka yake, apewe fursa ya kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote
watasomewa mashtaka, watasikiliza na kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili,
lakini hatua zitachukuliwa mara baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,” alieleza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KINANA ATOA MASHARTI ENDAPO RAIS MAGUFULI ATAMHITAJI AENDELEE KUWA KATIBU MKUU WA CCM”
Post a Comment