Monday, February 24, 2014


 NYONGEZA YA POSHO YAGONGA MWAMBA
 

 Madai ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutaka nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge hilo yamegonga mwamba. 

Habari kutoka ndani ya kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho ili kufuatilia madai hayo, zimedai kuwa baada ya uchunguzi wa kina, wajumbe wa kamati hiyo hawakuona sababu ya kupendekeza posho hizo kupandishwa.

Taarifa hizo zilidai kuwa wajumbe hao wamefikia uamuzi huo baada ya kupitia viwango vya posho vinavyolipwa na  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali na Mashirika ya Umma.

Pia kamati hiyo ilichambua viwango vya posho walivyolipwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na viwango vya posho ya kujikimu vya Sh80, 000 kwa siku wanavyolipwa watumishi wa Serikali.

 “Hili jambo linahitaji busara sana na kutazama mazingira ya nchi pia, kwa hiyo wajumbe wale baada ya kuoanisha viwango vya posho vya taasisi mbalimbali wameona Sh300,000 zinatosha,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake kutajwa.

Mjumbe mwingine, ambaye pia hakutaka kutajwa, alisema kuwa watakaa zaidi kukamilisha taarifa ya utafiti wao, kabla ya kuikabidhi kwa Mwenyekiti Kificho.
Alisema pamoja na umuhimu wa kazi za mbunge, lakini isingekuwa rahisi kuongeza posho katika mazingira ya sasa, ambapo wananchi wanalia hali ngumu ya maisha.

0 Responses to “ ”

Post a Comment

More to Read