Sunday, April 13, 2014
HAKIMU AMTANDIKA RISASI MFANYABIASHARA JIJINI ARUSHA WAKATI WAKIGOMBANIA MWANAMKE.
Do you like this story?
HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo ya
Maromboso, David Shayo (40), anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa kwa
kosa la kumpiga risasi mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia, kwa kile
kinachodaiwa kuwa ni ugomvi wa kugombea mwanamke.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo
walidai lilitokea Aprili 9 mwaka huu, saa 4:00 usiku katika eneo la Kona
Nairobi barabara ya Dodoma katika manispaa ya jiji la Arusha.
Taarifa zinadai kuwa Shayo ambaye naye
amejeruhiwa kichwani wakati wakigombana ,alianza kumsaka raia huyo Yusuf Muktal
(37), katika eneo la makao mapya mara baada ya kudokezwa kuwa anatembea na
mpenzi wake.
Hata hivyo haijafahamika jina na
mwanamke huyo anayedaiwa kusababisha ugomvi huo.
Mashuhuda ambao hawakutaka majina yao
kutajwa walisema hakimu huyo ambaye alikuwa akinywa pombe katika baa moja eneo
la Makao Mapya, alionekana kuzidiwa na kilevi na kuendesha gari kwa kasi
akimsaka Muktal katika maeneo mbalimbali ya jijini.
Aidha Shayo akiwa katika gari lake
alipata taarifa za kuwepo kwa Muktal eneo Makao Mapya, akiwa na mwanamke huyo
ndipo alipokwenda na gari lake lakini kabla ya kumfikia Muktal alipata taarifa
za kufuatiliwa na aliondoka eneo hilo akitumia gari lake.
Hakimu Shayo baada ya kufika eneo hilo
alianza kulifukuzia gari hilo na alipofika eneo la Kona Nairobi, alifanikiwa
kulisimamisha na baadaye wawili hao walisikika wakigombana.
Watoa taarifa walidai kuwa ugomvi huo
ulizidi kupamba moto na baadaye walisikia mlio wa risasi kwani hakimu huyo
alidaiwa alichomoa bastola na kumfyatulia risasi, kwenye mguu wa kushoto,
ambapo hadi sasa majeruhi amelazwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake Hakimu Shayo
akizungumza na gazeti hili wakati akihojiwa na polisi kituoni, alisema kuwa
alivamiwa na vibaka wakitaka kumpora baada ya yeye kusimama kwa lengo la
kumwokoa dereva wa gari aliyekuwa amepata ajali.
''Nililazimika kufyatua risasi hewani
kwa lengo la kuwatawanya vibaka waliovamia gari lililopata ajali kwa lengo la
kupora lakini bahati mbaya wakati kibaka mmoja alitaka kuninyang'anya bastola
risasi moja ilifyatuka na kumpiga (Muktal) mguuni,'' alisema.
Hakimu Shayo amefunguliwa kesi ya kujeruhiwa
kwa risasi yenye kumbukumbu namba AR/RB/4939/2014 na atafikishwa mahakamani
kujibu shitaka linalomkabili.
Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha,
Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
NA veronica Mheta, Arusha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “HAKIMU AMTANDIKA RISASI MFANYABIASHARA JIJINI ARUSHA WAKATI WAKIGOMBANIA MWANAMKE.”
Post a Comment