Monday, April 7, 2014

OPERESHENI SAFISHA JIJI YAIBUA LAWAMA NZITO.




WIKI moja baada ya Operesheni Safisha Jiji, baadhi ya wakazi wameomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq kuingilia kati, kuzuia uvunjifu wa sheria wa kubomolewa baadhi ya nyumba za watu wasiohusika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wakazi hao walisema kama opersheni hiyo ikiachwa ifanyike bila kufuata sheria, kuna hatari  ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na matokeo yake yakawa mfano wa ile ya Operesheni Tokomeza Ujangili.

Walisema wasiwasi huo unatokana na baadhi ya askari kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu kwa kuagiza nyumba za watu zivunjwe huku wakiondoka na baadhi ya mali kusikojulikana.

Walieleza hawana tatizo na operesheni hiyo, bali wameitaka Kamati ya Ulinzi ikiwa chini ya Mkuu wa Mkoa kuzingatia lengo maalumu la operesheni hiyo.

Mkazi wa Mtaa wa Livingston, aliyejitambulisha kwa jina moja la Amina, alisema kipande cha mbele cha nyumba yake kimevunjwa bila sababu za kueleweka, kwani yeye si mfanyabiashara.

“Namuomba Mkuu wa Mkoa awe makini kwa sababu kuna askari ambao walikuwa wanaipinga operesheni hii, sasa isije ikawa wanaihujumu kwa makusudi ili isimamishwe wapate kuendelea na ufisadi wao wa kujipatia fedha chafu kutoka kwa wamachinga,” alisema Amina.

Alisema ushahidi wa watu kubomolewa nyumba zao kinyume cha sheria upo, kwa kuhakikisha hilo ni vema mkuu wa mkoa akafanya ziara ya kujionea mwenyewe matukio hayo.

James Christopher, mkazi wa mtaa huo, alisema nyumba yake iko kwenye eneo rasmi na wala haijawekwa alama ya X, lakini imebomolewa na askari hao.

>>>Tanzania Daima

0 Responses to “OPERESHENI SAFISHA JIJI YAIBUA LAWAMA NZITO.”

Post a Comment

More to Read