Saturday, April 19, 2014
UCHAMBUZI WA MECHI ZA KUFUNGA PAZIA LIGI KUU BARA HUU HAPA!!.
Do you like this story?
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati leo (Aprili 19 mwaka huu) kwa
timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam fc wakikabidhiwa kombe
lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.
Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa
10 kamili jioni.
Mtandao huu unajaribu kukupatia
tathmini ya mechi zote saba zikazopigwa leo hii.
YANGA SC VS SIMBA SC
Mechi hii haina mchecheto sana
kwasababu timu zote zimeshapoteza nafasi ya ubingwa, japokuwa lengo kubwa leo
hii ni kutafuta heshima kwa klabu zote.
Simba wamefanya vibaya msimu huu na
kuelekea kuishia nafasi ya nne ambayo inategemeana na matokeo watakayopata
dhidi ya Yanga, wakati huo huo matokeo ya Kagera Sugar waliopo nyuma yao
yakisubiriwa huko Mkwakwani.
Simba wamecheza mechi 25 na
kujikusanyia pointi 37 katika nafasi ya nne, wakati Yanga wapo nafasi ya pili
kwa pointi 55 kwa kucheza mechi 25.
Endapo Yanga watashinda leo, basi
watafikisha pointi 58, lakini hazitawasaidia kitu zaidi ya kulinda heshima,
kwasababu Azam fc walishazivuka na kuchukua taji msimu huu.
Kwa mazingira haya matokeo ya ushindi
kwa timu yoyote hayatakuwa na maana hususani kwa Yanga, lakini angalau Simba
yanaweza kuwahakikishia kushika nafasi ya nne.
Makocha wa timu hizi, Dravko
Logarusic ( Simba) na Hans Van der Pluijm ( Yanga) wanakutana kwa mara ya
kwanza katika mechi ya watani wa jadi.
Lakini Loga aliwashawahi kuonja raha ya
ushindi desemba 21 mwaka jana baada ya kuwafunga Yanga mabao 3-1 kwenye mechi
ya `Nani Mtani Jembe`.
Pluijm leo ndio mara yake ya kwanza
kukutana na presha ya mechi ya watani wa jadi.
Yanga na Simba zinakutana zikiwa na
malengo yanayofanana, ingawa Simba wanakuwa kwenye presha kubwa zaidi.
Kama kweli wamedhamiria kupata nafasi
ya nne, basi ni muhimu kushinda kwasababu wakifungwa wataipoteza endapo Kagera
Sugar watashinda.
Kwa ujumla heshima ni muhimu sana na
ndio maana timu hizi zilijificha kambini ambapo Simba walijichimbia Zanzibar na
Yanga walikuwa Kunduchi jijini Dar es salaam.
Kwahiyo mechi hii itakuwa na ushindani
mkubwa na timu yoyote inaweza kushinda.
JKT RUVU V AZAM
FC
Mechi hii itapigwa katika uwanja wa
Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itatumika kuwakabidhi Azam fc
ubingwa wao wa kwanza waliofanikiwa kuutwaa.
Kwa mechi 25 walizocheza, Azam fc
hawajafungwa hata mechi moja, na leo hii wanahitaji kushinda ili kuandika
historia ya kubeba taji lao la kwanza bila kufungwa.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog
amewataka wachezaji wake kucheza kwa kujituma ili kushinda mechi ya leo na
kushangilia ubingwa kwa raha zote.
Baada ya mechi hii, Azam fc wameandaa
sherehe za kushangilia ubingwa wao huko Chamazi, hivyo ushindi utanogesha
zaidi.
Kwasababu hii ya Azam kutaka kuandika rekodi,
mechi hii itakuwa ngumu kwa kocha wa JKT Ruvu, Fredy Minziro.
Hata hivyo kama Minziro atapoteza mechi
hii haitakuwa na madhara kwake kwasababu poiniti 31 alizonazo sasa katika
nafasi ya 10 zinamfanya awe mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kwa ujumla mechi itakuwa na mvuto
kwasababu Azam fc wanahitaji kushinda.
TANZANIA PRISONS VS ASHANTI
UNITED
Hii ni mechi ngumu mno na inahitaji
maarifa makubwa kwa kocha wa Ashanti, Mzee Abdallah Kibadeni na David Mwamwaja
wa Tanzania Prisons.
Kati ya timu hizi mbili, moja lazima
iungane kushuka daraja na timu za JKT Oljoro ya Arusha na Rhino Rangers ya
Tabora.
Timu zote zimecheza mechi 25 na
kujikusanyia pointi 25. Kinachozitofautisha ni mabao ya kufunga na kufungwa.
Prisons wamecheza mechi 25 ambapo
wameshinda mechi 5, sare 10 na kupoteza mechi 10.
Wajelajela hao wamefumania nyavu mara
25 na kufungwa mabao 33. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa unapata hasi (-8).
Ashanti United wameshinda mechi 6, sare
7 na kufungwa mechi 12.
Wamefunga mabao 20 na kufungwa mabao
38. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa anapata hasi kumi na nane (-18).
Kwa wastani huo wa mabao ya kufunga na
kufungwa, Prisons wanakuwa juu ya Ashanti United.
Katika msimamo, Prisons wapo nafasi ya
11, huku nafasi ya 12 ikikaliwa na Ashanti United, lakini zimefungana pointi.
Kuelekea katika mechi hiyo, klabu zote
zinahitaji ushindi, lakini Ashanti ndio wahitaji wakubwa zaidi kwasababu
wamezidiwa mabao mengi ya kufunga na Prisons.
Endapo Ashanti United watashinda mechi
hiyo watafikisha pointi 28 na kuvuka mkasi wa kushuka daraja, wakati Prisons
watakuwa wameshashuka daraja.
Matokeo ya sare ya aina yoyote ile
yatawashusha daraja Ashanti kwasababu ya wastani wa mabao ya kufunga na
kufungwa.
Kama Prisons watapata sare siku ya leo,
watakuwa wamenusurika kushika daraja kwa faida ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kitendawili cha timu gani inashuka
baina ya Prisons na Ashanti United kitageguliwa kesho uwanja wa Jamhuri mkoani
Morogoro.
MBEYA CITY FC VS MGAMBO JKT
Hii itakuwa mechi muhimu kwa kocha mkuu
wa klabu hiyo ya Mbeya City fc, Juma Mwambusi kutokana na matokeo
aliyoyapata wiki iliyopita dhidi ya Azam fc ambapo alifungwa mabao 2-1 nyumbani
na kuwapa ubingwa rasmi.
Endapo Mwambusi atashinda mechi hii,
basi itakuwa faraja kubwa kwake na kwa mashabiki wa klabu hiyo iliyoleta
ushindani mkubwa mno msimu huu.
Mbeya City FC mpaka sasa wamecheza
mechi 25 na kujikusanyia pointi 46 katika nafasi ya tatu ambayo tayari
wamefanikiwa kuichukua.
Kwa upande wa Mgambo JKT, wanauchukulia
mchezi huo kwa uzito wa hali ya juu ili kuweza kupata pointi tatu muhimu na
kufikisha pointi 29.
Japokuwa maafande hawa wapo nafasi ya
10 baada ya kucheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 26 na kujiweka mazingira
mazuri ya kubaki ligi kuu, lakini bado wanahitaji ushindi katika mechi ya leo.
Kwa mazingira haya, mechi hii itakuwa
na mvuto mkubwa na soka la ushindani linatarajiwa.
COASTAL UNION VS KAGERA SUGAR
Katika mechi hii itakayopigwa uwanja wa
Mkakwani, timu zote zinaingia kwa mitazamo tofauti.
Coastal Union hawana cha kupoteza,
lakini wakishinda wanaweza kusogea nafasi moja mbele kutegemeana na
matokeo watakayopata Mtibwa Sugar leo hii.
Wagosi wa Kaya waliotabiriwa kufanya
makubwa msimu huu wamedoda katika nafasi ya 9 kwa pointi 29 baada ya kucheza
mechi 25.
Mtibwa wapo nafasi ya 8 kwa pointi 30,
hivyo wakifungwa leo hii wataporomoka nafasi moja chini.
Kagera wao wanahitaji pointi tatu
muhimu ili angalau kuambulia nafasi ya nne, lakini kama Simba watafungwa leo
ndio itawasaidia.
Kagera wapo nafasi ya 5 kwa pointi 35
na kama watashinda watafikisha 38, na kama Simba wenye pointi 37 watafungwa,
basi watachukua nafasi ya nne.
Kwa mazingira haya, Kagera Sugar
watakuwa washindani wazuri leo hii na kuufanya mchezo uwe na mvuto.
RHINO RANGERS VS RUVU SHOOTING
Mechi hii haitegemewi kuwa ya ushindani
hata kidogo kwasababu matokeo ya ushindi yatawasaidia Ruvu Shooting
kusogea nafasi ya juu kutoka ya 6 kwenda ya 5.
Ruvu Shooting wapo nafasi ya 6 katika
msimamo wakiwa na pointi 35 swa na Kagera, lakini Wakata miwa wana wastani
mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kama Kagera na Simba zitafungwa leo,
halafu Ruvu Shooting wakashinda, basi watafanikiwa kuchukua nafasi ya 4.
Rhino walishashuka daraja, hivyo hawana
wanachokitafuta leo hii zaidi ya kukamilisha ratiba tu.
Kwa ujumla mechi hii itakuwa na presha
kwa Ruvu Shooting kwasababu watakuwa wanahitaji matokeo mazuri huku wakiwaombea
mabaya Simba na Kagera.
JKT OLJORO V MTIBWA SUGAR
Mechi hii haina jipya kwasababu Oljoro
wameshashuka daraja msimu huu.
Mtibwa watahitaji ushindi ili kuendelea
kukaa nafasi yao ya nane.
Kwa ujumla mechi hii haitakuwa na
msisimko hata kidogo na mpira wa kawaidia unategemewa, japokuwa Mtibwa wanaweza
kuingia kwa nguvu.
Mtandao huu utakuletea matokeo ya mechi
zote hapo baadaye.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UCHAMBUZI WA MECHI ZA KUFUNGA PAZIA LIGI KUU BARA HUU HAPA!!.”
Post a Comment