Saturday, April 12, 2014

UFALME WA RAGE SIMBA WAFIKA KIKOMO, SWALI NANI KURITHI MIKOBA YAKE?, KAZI KWA WANACHAMA!!




KWA MUDA mrefu mashabiki  na wanachama wa Simba sc wamekuwa wakiamini kuwa klabu yao imefika hapo ilipo kwasababu ya mwenyekiti wao Ismail Aden Rage kuongoza vibaya.

Rage amekuwa akisuguana na wanachama wake kwa muda mrefu, lakini sasa ameshatangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mei 4 mwaka huu.

Rage alitangaza maamuzi hayo machi 16 mwaka huu katika mkutano mkuu wa wanachama  ulioitishwa maalumu kwa ajili ya kufanya marekebisho wa katiba.
Kauli ya aina yake katika mkutano huo ilikuwa ile ya Rage kuwaita wanachama wa Simba ni  ‘mbumbumbu’
Kufuatia kauli hiyo, Rage, alilazimika kuwaomba radhi wanachama hao zaidi ya 571 waliohudhuria mkutano huyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

“Napenda kuwaomba radhi wanachama wenzangu kutokana na nilivyosema tuache umbumbumbu, lakini sikuwa namaanisha kama wengi wenu mlivyoelewa,” alisema Rage.

Licha ya kusema hatagombea tena uongozi, Rage, alisema ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Simba na atatoa mchango wake ili kufanikisha maendeleo.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kauli hiyo, Rage alishawahi kusema kauli za aina yake.
Mwezi machi mwaka jana aliwahi kuuita  mkutano wa wanachama walioaminika kuwa zaidi ya 600 ambao ulitangaza kumpindua madarakani  kuwa ni kama `kikao cha harusi`.

Pia novemba mwaka jana kamati ya utendaji ya Simba ilitangaza kumuondoa madarakani mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.

Kamati hiyo ilifikia uamuzi wa kumsimamisha Rage akiwa nje ya nchi  na kumtangaza aliyekuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ kushika nafasi hiyo ya juu zaidi katika klabu hiyo.

Mzee Kinesi alisema walifikia maamuzi hayo kutokana na mwenyekiti huyo kwenda kinyume na makubaliano na Kamati ya Utendaji ya Simba.

Lakini baadaye ya mwanaume huyo kurudi alitamba kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa Simba na kikao hicho kilikuwa kikao cha harusi.

Wakati anawasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na kundi kubwa la watu walioaminika kuwa wanachama wa Simba waliojitokeza kumlaki na kumshangilia kwa nguvu.

Kweli jamaa alirudi na baadaye TFF walitangaza kumtambua kuwa ndiye mwenyeki halali wa Simba, lakini wakamtaka aitishe mkutano wa dharura na kumpangia ajenda.
Rage aligoma na kusema yeye ndiye mwenye mamlaka ya kupanga ajenda za mkutano kwa mujibu wa katiba.
Yapo mengi ya kuyasema kuhusu Rage, lakini sasa ameshatangaza kung`atuka baada ya muda mrefu wa mvutano na viongozi wenzake pamoja na wanachama wa Simba.

0 Responses to “UFALME WA RAGE SIMBA WAFIKA KIKOMO, SWALI NANI KURITHI MIKOBA YAKE?, KAZI KWA WANACHAMA!!”

Post a Comment

More to Read