Saturday, April 12, 2014
KWA HILI PRISONS WANA POINTI, TFF `FIGISUFIGISU` ZA NINI KWENYE MAMBO YA MSINGI?
Do you like this story?
HAKUNA jambo baya kama kujijengea mazingira ya kutoaminiwa kwa maamuzi
yako hasa unapokuwa kiongozi mwenye dhamana ya kuongoza taasisi, chama, idara
na sehemu nyingine za kazi.
Ukiwa kiongozi inaweza kufika
wakati ukakaa na viongozi wenzako na kufikia maamuzi fulani baada ya
kujadiliana, lakini unapowasilisha kwa watu wanaohusika na maamuzi hayo
akajikuta unawaumiza na kushindwa kukuamini.
Niliwahi kufunndishwa kuwa moja ya sababu ya migogoro mingi katika
jamii ni kukosekana kwa mawasiliano baina ya pande mbili zinazohusika katika
jambo fulani.
Mawasiliano na watu unaowaongoza ni muhimu sana ili kuepukana na lawama
zisizo za msingi.
Kila kitu hutokea kwasababu fulani, lakini unaposhindwa kubainisha
sababu ya kufikia maamuzi yako, husababisha jamii inayokuzungukoa kushindwa
kukuamini.
Kwasasa ligi kuu soka Tanzania bara imefikia hatua ya mwisho ambapo
kama kawaida imejigawa katika makundi matatu.
Mosi; kuna timu ambazo zinachuana katika kinyang`anyiro cha ubingwa.
Hapa unawazungumzia wanaume wawili, vinara Azam fc na mabingwa
watetezi, Dar Young Africans.
Azam fc wapo kileleni kwa pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, wakati
Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 52 kufuatia kushuka dimbani mara 24.
Ubora wa Azam fc umewafanya wasifungwe katika mechi 24 walizocheza
mpaka sasa.
Mchuano huu mkali unaweza kufika tamati hapo kesho majira ya saa 12
jioni.
Timu zote mbili zitashuka dimbani a
mbapo Yanga watakuwa wageni wa maafande wa JKT Oljoro katika uwanja wa
Shk. Amri Abeid, mjini Arusha.
Azam fc watakuwa na kibarua dhidi ya Mbeya City katika dimba la Sokoine
,jijini Mbeya.
Kwanini nasema biashara ya kusaka ubingwa inaweza kumalizika kesho?
Sababu si nyingine bali ni kama Azam fc watashinda mechi yao, rasmi watakuwa
wamewavua ubingwa Yanga msimu huu.
Wana Lambalamba hao wakishinda watafikisha pointi 59 kileleni ambazo
Yanga hata wakishinda mchezo wao wa kesho na wa mwisho dhidi ya Simba
hawataweza kufikisha pointi 59.
Kwa maana hiyo kesho ni siku nzuri ya kufuatilia hatima ya Azam fc
katika harakati zake za kuchukua taji kwa mara ya kwanza, wakati Yanga wakiwa
katika presha ya kutetea mwari wao.
Mbeya City wao wanaisaka nafasi ya tatu katika msimu wao wa kwanza
tangu wapande ligi kuu, hata hivyo wameshaichukua kwasababu hakuna timu yoyote
ya chini inayoweza kufikisha pointi 47 walizonazo mpaka sasa.
Kuelekea katika mechi za kesho, tayari mengi yameshasemwa sana ikiwemo
Azam fc kuaminika kuwahonga Mbeya City ili wawape ushindi wa chee.
Jana niliandika kuhusiana na jambo hili, hivyo unaweza kurejea katika
habari zetu kwenye mtandao huu.
Pili; zipo timu zinazosaka nafasi nzuri katika msimamo. Hapa unakutana
na Simba sc, Kagera Sugar, Mtibwa sugar, Ruvu Shooting, na Coastal Union . Hizi
hazina presha kubwa kwasababu zina uhakika wa kubakia ligi kuu.
Tatu; kuna kundi la kifo, hakika hizi timu zinachuana vikali kukwepa
kushuka daraja.
Angalau JKT Ruvu na Mgambo wanaonekana kujitahidi kujikwamua kwasababu
wamevuka pointi 24.
Mgambo wapo nafasi ya 10 kwa poiniti 25 baada ya kucheza mechi 24,
wakati JKT Ruvu wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 kufuatia kucheza mechi 24.
Lakini unapozungumzia Prisons na Ashanti zenye poiniti 22 kila moja
katika nafasi za 11 na 12 unazungumza jambo muhimu sana.
Timu hizi zinachuana vikali ili kupata klabu moja itakayoungana na
Rhino Rangers na JKT Oljoro kushuka daraja msimu huu.
Taarifa ya shirikisho la soka Tanzania iliyotumwa kwa vyombo vya habari
jana ilieleza kuwa leo kutakuwa na mechi tatu za ligi kuu soka Tanzania bara
ambapo Simba wataumana na Ashanti United uwanja wa Taifa, Prisons dhidi ya
Rhino Rangers uwanja wa Sokoine, halafu Coastal Union na JKT Ruvu uwanja wa
Mkwakwani.
Lakini muda mfupi baadaye ilitumwa taarifa ya marekebisho ya ratiba
ambapo mechi ya Simba na Ashanti United ilisogezwa mpaka kesho jumapili.
Kwa bahati mbaya sana haikuelezwa sababu za kusogeza mechi hiyo kutoka
leo hii kwenda kesho.
Haikuelezwa kama uwanja wa Taifa utakuwa na shughuli nyingine au kuna
sababu zozote za kiusalama kwa timu zote.
Kila mtu alisema lakwake, wengine wakasema ni kuhofia mvua
zinazoendelea kunyesha kuanzia jana.
Lakini wakahoji kama ni hivyo, nani anayeweza kujua kama leo kutakuwa
na mvua uwanja wa Taifa?.
Kimsingi kila mtu anasema ya kwake. Sikuona haja ya kuwatafuta TFF
kwanini wameahirisha mechi hiyo hata bila wao wenyewe kutoa sababu ya moja kwa
moja.
Lengo langu si kutaka kuandika juu ya sababu ya kuahirisha mechi hiyo,
bali ni udhaifu walionao katika suala la mawasiliano na kuwafanya waonekane
wanaleta `figisufigisu`.
Labda watasema sababu wakishinikizwa na vyombo vya habari au wakuu wa
juu ndani ya TFF, lakini najua ilikuwa ni muhimu kwao kuwasiliana na umma
kuueleza kwanini mechi hiyo inasogozwa mbele, kwa lugha nzuri kwanini
inaahirishwa.
Hapa ndipo dhana ya mawasiliano inapokuja. Kama TFF wangesema mapema,
au kueleza sababu za kuahirishwa kwa mechi hiyo wangeeleweka mapema kuliko
kukumbatia sababu yao na kuonesha kama wana ubabe au mamlaka ya kuamua
watakavyo na si kuwafikiria waathirika.
Ona sasa wanavyojijengea mazingira ya kutoaminiwa na jamii yao.
Kwa anayefuatilia vyombo vya habari,
jana Tanzania Prisons wamekerwa mno na mabadiliko haya ya ratiba.
Hoja ya Prisons ilikuwa kama yangu tu, kwanini mechi imeahirishwa
ghafla na nani mwenye mamlaka ya kuahirisha mechi iliyopangwa.
Inspekta Sadick Jumbe, katibu mkuu wa Prisons alisema wameshangazwa
sana na maamuzi hayo ya Bodi ya ligi kwasababu wanataka kupanga matokeo.
Sheria zipo wazi hasa ile ya kuahirisha mechi ambao kuna kipengele
kinahusu majanga ya asili ambayo si mpango wa binadamu.
Mfano kama kuna mvua kubwa kama ili ye Mabatini jumatano, mwamuzi anayo
mamlaka ya kuahirisha mechi mpaka siku nyingine itakayopangwa.
Kwa hii ya Prisons haikufikia hatua hiyo, kibaya zaidi walioahirisha
hawajasema kwanini.
Prisons wanaona kama TFF wanapanga matokeo kwasababu wanajua wazi kuwa
Ashanti ni wapambanaji wenzao wa kukwepa daraja.
Ilikuwa jambo nzuri kwa mechi za klabu hizi kuchezwa kwa wakati mmoja
ili kuepuka kumpa nafasi mwenzake kujua matokeo ya mapema.
Kama Prisons anacheza leo, manake Ashanti watakuwa wanawasikilizia
wanafanya nini na wao waingiaje kesho uwanjani dhidi ya Simba sc.
Kwa sababu za Prisons, nadhani jamaa wana pointi ndani yake.
TFF lazima wabadilike sana hasa katika kuchukua maamuzi muhimu
yanayogusa maslahi ya kundi fulani.
Hakuna sababu ya kuendelea kutoa taarifa bila sababu. Kama kuna sababu
kubwa ya kuahirishwa kwa mechi hiyo, kulikuwa na ubaya gani kuisema mapema ili
hata Prisons wajiridhishe.
Hivi kweli waliwasiliana na Prisons mapema juu ya mabadiliko hayo?, au
ndio watu wachache walikaa na kuamua tu.
Kukosekana kwa mawasiliano ni kujijengea mazingira mabaya ya kuwa una
ajenda za siri.
Wakati huu ambao ligi inafikia tamati, kashfa ya kupanga matokeo huwa
inajitokeza, hivyo TFF kuweni makini na mechi zinazohusisha timu zinazotafuta
ubingwa na kushuka daraja.
Jambo nzuri ni kujenga utataribu kwa kujibu swali la kwanini?
Kama mechi inasogezwa mbele au inaahirishwa, eleza kwanini?.
Kama unachukua maamuzi fulani unayodhani yana maslahi, weka wazi
kwanini?
TFF kama wataendelea kutokuwa makini watalaumiwa sana kama hili la
Prisons ambalo hawakubainisha kwanini wamesogeza mechi.
Kama watatoa sababu, basi ni
baada ya kushituliwa, lakini toka awali hawakueleza katika taarifa yao zaidi ya
kusema mechi itachezwa kesho jumapili.
Prisons wana pointi, TFF fikirieni sana ili siku zijazo mjiepushe na
maamuzi kama haya bila kuwasilina na
wahusika na inafika muda hawajui kwanini jambo fulani limetokea.
Rais Jamal Malinzi, jamii ya watu wa mpira bado ina imani kubwa na
wewe. Jaribu kurekebisha kasoro kama hizi ili kujiepusha na kashfa ndogo ndogo
kama hizi.
Kuna watu wachache watakaokuharibia taswira yako bila sababu ya msingi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KWA HILI PRISONS WANA POINTI, TFF `FIGISUFIGISU` ZA NINI KWENYE MAMBO YA MSINGI?”
Post a Comment