Saturday, April 12, 2014

WATU 37 WAKAMATWA VURUGU ZA BODABODA MBEYA.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi





Na David Nyembe


Watu 37 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa mbeya kwa kosa la kufanya fujo na kuharibu mali.

Akizungumzia Tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amesema kuwa tukio hilo limetokea April 11 mwaka huu  majira ya  saa 10:30 asubuhi huko katika eneo la iyela - airport, kata ya  iyela,   jijini Mbeya   ambapo kundi la watu wakiwemo waendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda zaidi ya  mia mbili walivamia kwenye msiba wa marehemu siza john mwambenja [28]  mwendesha pikipiki @ bodaboda, mkazi wa airport  na kufanya fujo ikiwa ni pamoja na kuharibu mali mbalimbali katika nyumba hiyo.

Amesema Lengo la Bodaboda hao ilikuwa kushinikiza kumkamata mtalaka wa marehemu Ndugu Oliva herode mwamlima [ 25] mkazi wa forest mpya ambaye alikuwepo katika msiba huo kwa madai kuwa anahusika na njama za mauaji ya  aliyekuwa mume wake kutokana na kuachwa kwa sababu za matatizo ya kifamilia.

Amesema kuwa Marehemu Siza Johnjohn  aliuawa na mtu/watu wasiofahamika na mwili wake kukutwa umetupwa kando ya reli ya tazara  tarehe 09.04.2014 ukiwa na jeraha la kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kando yake kutelekezwa pikipiki yake mpya yenye namba za usajili t. 932 ctz aina ya  kinglion.

Kamanda Msangi amebainisha kuwa Kufuatia vurugu hizo zilizozimwa na jeshi la polisi mkoa wa mbeya, watu 37 walikamatwa na kufikishwa mahakama ya mwanzo mbeya mjini ambao walisomewa mashitaka yao shauri la jinai namba 291/2014. 

Watuhumiwa wote wamepelekwa mahabusu gereza la ruanda ambapo kesi itaanza kusikilizwa 14.04.2014.

Aidha katika vurugu hizo mali za jeshi la polisi gari moja la kituo cha polisi kati  474 aina ya  land rover 110  liliharibiwa kwa kupigwa mawe na kuvunjwa kioo kikubwa cha mbele. Hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa kutokea wakati wa vurugu hizo na hali ya amani ilirejea kuwa ya kawaida na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kamanda wa polisi mkoa wa mbeya kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi ahmed z. Msangi anatoa  wito kwa jamii kuacha tabia ya  kujichukulia sheria mkononi badala yake wahakikishe wanawafikisha katika mamlaka husika watuhumiwa wanowakamata kwa tuhuma mbalimbali ili hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe.

Aidha anatoa rai kwa jamii kujenga tabia ya  kuheshimu mamlaka zilizowekwa kisheria ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola ili kuepuka matatizo yanayoweza kuepukika badala ya kuleta ushindani na vurugu. Pia kamanda msangi amesisitiza kuwa jeshi la polisi halitasita kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaokaidi na kuleta vurugu.

0 Responses to “WATU 37 WAKAMATWA VURUGU ZA BODABODA MBEYA.”

Post a Comment

More to Read