Thursday, May 15, 2014

PINDA ATANGAZA VITA NA MAMEYA,WENYEVITI WANAOKUZA MIGOGORO.




Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema ataanza kuwavua madaraka mameya na wenyeviti watakaobainika kukuza migogoro ndani ya halmashauri zao kwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Alitoa rai hiyo jana wakati akifungua mkutano wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat) unaofanyika jijini hapa.
Amesema baadhi ya mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya wamekuwa wakiweka mbele masilahi binafsi kwa kukuza migogoro na hatimaye muda mwingi kutumika kwenye migogoro huku shughuli za maendeleo zikisimama.

“Mkigombana wote tunawaondoa. Msiendekeze migogoro kwenye halmashauri zenu. Acheni kutumia muda mwingi kulumbana na kugombana. Mnakuza mambo ambayo hayana masilahi kwa maendeleo ya wananchi,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu alitoa mfano wa mgogoro uliosababisha meya wa Manispaa ya Bukoba kujiuzulu, akisema kuwa ulimalizika baada ya mwenyewe kutangaza hivyo, lakini baadaye madiwani wa kambi yake walienda mahakamani kuzuia vikao, jambo lililosababisha fedha za maendeleo kushindwa kupelekwa.

Amesema Tanzania ipo katika mkakati wa kuifanya iwe miongoni mwa nchi zenye uchumi bora duniani ifikapo mwaka 2025 na sehemu kubwa ya maendeleo inatekelezwa katika ngazi ya Serikali za Mitaa, hivyo ili kufikia lengo hilo hawezi kuvumilia kuona baadhi ya mameya na wenyeviti wakikwamisha maendeleo kwenye maeneo yao.

Kuhusu elimu, Pinda alisema kwenye shule za msingi kuna upungufu wa madawati 1,494,895 hivyo Alat inatakiwa kutokwepa jukumu hilo na kutumia fursa zilizopo kuhakikisha yanachongwa.
“Hivi Alat mnakubali aibu hii ya watoto wa wananchi wenu kukaa chini kwenye udongo? Hii haikubaliki, lazima mtimize wajibu wenu wa kuhakikisha kila halmashauri inayatengeneza,” alisema Pinda.
Pinda pia aliiagiza Alat kutia msukumo kwenye ujenzi wa nyumba bora za wananchi ili waondokane na kuishi kwenye nyumba zilizoezekwa nyasi.

Mwenyekiti wa Alat, Dk. Didas Masaburi alisema wakati inatimiza miaka 30 jumuiya hiyo imefanikiwa mambo mengi, ikiwamo kusimamia matumizi ya fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo kwenye halmashauri nchini.

0 Responses to “PINDA ATANGAZA VITA NA MAMEYA,WENYEVITI WANAOKUZA MIGOGORO.”

Post a Comment

More to Read