Thursday, May 15, 2014

SERIKALI INAFANYA MZAHA NA UGONJWA WA DENGUE


Waombolezaji wakibeba jeneza lenye mwili wa Daktari Gilbert Buberwa wa Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kuagwa. Daktari huyo, aliyefariki kwa kuugua homa ya dengue. Picha na Rafael Lubava 


Nchi nzima imekumbwa na taharuki kutokana na watu zaidi ya 400 kuugua homa ya dengue na tayari watu watatu wamepoteza maisha, akiwamo daktari bingwa wa magonjwa ya akili aliyekuwa akifanya kazi Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam. Hofu hiyo kwa kiasi kikubwa imetokana na habari kwamba ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo na husababishwa na aina ya mbu ajulikanaye kama aedes, ambaye husambaza maradhi hayo nyakati za mchana.

Kinachotia hofu zaidi ni mwenendo usioridhisha wa Serikali ambayo imekuwa kama mtazamaji katika kupambana na ugonjwa huo. Badala ya kuongoza na kuonyesha njia, kwa maana ya kubuni mikakati ya kupunguza kasi ya ugonjwa huo na kutoa taarifa za uhakika na kwa wakati kwa wananchi, Serikali imejenga taswira ya kutokuwa na uwezo katika mapambano hayo. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilisema juzi kwamba itapeleka taarifa za kuwapo kwa ugonjwa huo nchini katika Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mwongozo wa kanuni za afya za kimataifa unavyoelekeza.

Kitu muhimu hapa ni aina ya taarifa zitakazotumwa kwa shirika hilo, kwani kulitaarifu tu kuhusu uwapo wa janga hilo hapa nchini siyo muhimu kwa kuwa tayari suala hilo linajulikana. 

Kinachotakiwa ni taarifa zenye takwimu sahihi, ikiwa ni pamoja na idadi kamili ya watu walioambukizwa na maeneo wanakotoka. Tunasema hivyo kutokana na takwimu zilizotolewa na Serikali kutiliwa shaka na kukosa uhalisia kulingana na ukubwa wa tatizo.

Kwa mfano, inakadiriwa kwamba idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa huo ni kubwa mno kulinganisha na idadi ya watu 400 nchi nzima iliyotajwa na Serikali juzi. Taarifa tulizonazo ni kwamba Hospitali ya Mwananyamala pekee imepata wagonjwa wapatao 300 kati ya Aprili na mwezi huu.

Ofisi ya WHO iliyopo jijini Dar es Salaam jana ilitoa tahadhari kwamba dengue sasa ni janga na kuonya kuwa, zisipopatikana takwimu sahihi za ugonjwa huo nchi nzima, hali itakuwa mbaya sana baadaye. WHO ilisema ugonjwa huo ni suala mtambuka, kwa maana ya kuzigusa wizara nyingine nyingi, hivyo isiachiwe Wizara ya Afya pekee, bali pia wizara zinazohusika na miundombinu, maji, ujenzi na kadhalika lazima zihusishwe.

WHO inasema pia kwamba lazima utafiti ufanyike ili kujua tabia za mbu hao na virusi vipi vimesambazwa kulinganisha na maeneo mengine yenye ugonjwa huo. Dengue iliingia nchini mwaka 2010 na kuua baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Serikali haikutaka kuufahamu ugonjwa huo na hivi sasa ndipo taasisi zake kama Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS) na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) zinahaha kufanya tafiti ili kuufahamu na kuishauri Serikali.

Tunaitaka Serikali ielekeze nguvu zake katika kuutokomeza ugonjwa huo. Zinahitajika fedha nyingi, vifaa na vitendea kazi vya kuchukulia vipimo na kutoa kinga kwa wauguzi na madaktari ili wasizidi kuambukizwa na kupoteza maisha. Vipimo visitozwe fedha ili kunusuru maisha ya wagonjwa wasio na uwezo kifedha. 

Ianzishwe operesheni maalumu kunyunyizia dawa katika mazalio ya mbu na kazi hiyo iwe endelevu badala ya zimamoto. Matarajio yetu ni kwamba Serikali haitafanya mzaha tena katika kupambana na homa ya dengue.

Chanzo;Mwananchi                                                                                            

0 Responses to “SERIKALI INAFANYA MZAHA NA UGONJWA WA DENGUE”

Post a Comment

More to Read