Thursday, May 15, 2014

UDA ZINAZOKATIZA SAFARI DAWA IMEIVA




Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Vyombo vya Majini na Ardhini (Sumatra) imeliamuru Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) kuandika maeneo ya safari kwenye mabasi yake kutokana na madai ya kukatisha safari.

Akizungumza na gazeti hili jana, meneja leseni wa Sumatra, Leo Ngowi alisema wamelazimika kutoa amri hiyo baada ya kupokea malalamiko ya usumbufu na gharama wanazopata abiria wanaotumia usafiri wa mabasi hayo sehemu mbalimbali za jiji.
“Nimezungumza na mmoja wa maofisa wa Uda na tumekubaliana kuanzia leo waanze kutekeleza utaratibu huo,” alisema na kuongeza:

“Tusingependa kusikia tena abiria wanapata mateso na usumbufu usio na ulazima kwa kutumia mabasi hayo.”
Baadhi ya madereva wa Uda wamedaiwa kukatiza ‘ruti’ kwa lengo la kukusanyia fedha nyingi.

“Abiria wanapata usumbufu ruti zinapokatizwa kwa kuwa hawafahamu mwanzo na mwisho wa maeneo ya safari zao,” alisema.

Ofisa wa Uda, Henry Bantu alipoulizwa kuhusu kupokea amri hiyo, hakuwa tayari kuelezea kwa kirefu akidai kwamba yeye siyo msemaji wa shirika.

“Mimi siyo msemaji, lakini nachoweza kukueleza ni kwamba tuko kwenye mchakato wa kuboresha huduma zetu,” alisema Bantu.
Tofauti na mabasi mengine yanayotoa huduma za usafiri Dar es Salaam kupangiwa rangi maalumu pamoja na kuandikwa maeneo ya safari zao mbele na mlangoni kuandikwa kiwango cha nauli, mabasi ya Uda hayana utaratibu huo.

Wakati huohuo, Ngowi amesema wamezifungia daladala 13 kutokana na kuwa kwenye hali ya uchakavu kiasi cha kutishia usalama wa abiria.

Alisema kiutaratibu, mabasi yanayotoa huduma lazima yawe kwenye hali nzuri ya usalama ili kuepusha usumbufu kwa abiria na hata kusababisha ajali.

“Hatutakubali kuona mabasi ya daladala yasiyokidhi sheria na taratibu za kubeba abiria yakiendelea kutoa huduma jijini Dar es Salaam,” alisema Ngowi.

0 Responses to “UDA ZINAZOKATIZA SAFARI DAWA IMEIVA”

Post a Comment

More to Read