Wednesday, May 14, 2014

WAZAZI MKOANI NJOMBE WATAKIWA KUWAPA MAHITAJI WANAFUNZI NA SI KUENDEKEZA ULEVI TU




Imeelezwa kuwa wazazi na walezi wengi mkoani Njombe wamekuwa wakithamini zaidi unywaji pombe kuliko kuwatimizia mahitaji watoto wao wanaosoma elimu ya awali na msingi, jambo linalochangia kudidimiza elimu kwa wanafunzi hao.

Hayo yamebainika katika kikao cha chama cha waalimu wa awali Tanzania (TPTO) mkoa wa Njombe na waalimu wa shule za awali na msingi kilichofanyika hii leo katika ukumbi wa kata ya Iwawa wilayani Makete.

Akichangia katika kikao hicho Mwalimu Frida Sanga kutoka shule ya msingi Makete amesema elimu ya Tanzania bado ina mapungufu kwa kuwa wanadharau elimu ya awali ambayo ndiyo yenye msingi wa elimu "Unakuta hata waalimu wanaofundisha madarasa ya awali hawathaminiwi, wanaonekana kama hawafanyi kitu chochote kile, msingi wa elimu upo kwa watoto hawa wa awali na hao waalimu wanaowafundisha wanatakiwa kuheshimiwa na kuungwa mkono na jamii nzima na serikali kwa ujumla na si kuwapuuza" amesema.

Kwa upande wake mwl Vintan Mbilinyi kutoka shule ya Msingi Maleutsi ameitaka serikali kuwa na ukaribu zaidi na waalimu wa elimu ya awali huku akiwashauri waalimu wanaosoma hivi sasa kusomea kufundisha madarasa ya chini badala ya kukimbilia madarasa ya juu

"Hawa vijana wa siku hizi hawataki kufundisha madarasa ya chini mfano darasa la awali au la kwanza na badala yake wanataka kuanzia la tano na kuendelea kwa kuwa hawataki shida, sisi tunaofundisha madarasa haya ya chini tuna shida sana" amesema

Mwenyekiti wa chama chicho cha TPTO mkoa wa Njombe Mwl. Magreth Nyika amesema ni kweli elimu ya awali ina changamoto nyingi hivyo ni wajibu wao kwa pamoja kujiunga kwenye chama chao ili nao watambulike na washirikiane kwa pamoja kutatua changamoto zinazowakabili.

Naye katibu wa chama hicho Mwalimu George Mjema amesema upo umuhimu wa waalimu kufanya semina kwa wazazi kuwaeleza ili waone tabu wanayowapa watoto wao pindi wanaposhindwa kuwahudumia na kuwapa mahitaji yote ya shuleni huku wengi wa wazazi wao wakionekana kuendekeza unywaji pombe.

Chama hicho cha TPTO mkoa wa Njombe kinaendelea kuwakusanya wanachama katika wilaya zote za mkoa huo kikiwa na kauli mbiu "sauti zetu zisikilizwe" ambapo mpaka sasa kina zaidi ya wanachama 114

0 Responses to “ WAZAZI MKOANI NJOMBE WATAKIWA KUWAPA MAHITAJI WANAFUNZI NA SI KUENDEKEZA ULEVI TU ”

Post a Comment

More to Read