Thursday, June 19, 2014

MATANGAZO YA WAGANGA WANAOTIBU UKIMWI YAWAVUNJA MOYO WATAFITI



MATANGAZO ya waganga wa jadi wanaotibu ukimwi kwa dawa za asili, yanawavunja moyo watafiti na wanasayansi wanaoendelea kutafuta tiba ya ugonjwa huo.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mjamzito au anayenyonyesha kwenda kwa mtoto uliofanyika viwanja vya Tangamano jijini hapa.

Alisema matangazo hayo yanawatia hofu wananchi na kuamini kuwa serikali na wataalamu wa afya wameshindwa kutafuta tiba ya ugonjwa huo huku yakichochea ngono.

“Tatizo hili limechangia kuongezeka kwa waathirika wengi wa ukimwi… iwapo hatutachukua hatua za kudhibiti kwa haraka, kuna uwezekano wa serikali kushindwa kuwahudumia waathirika wa ungonjwa huo,” alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita, alisema ni asilimia 21.9 ya wanaume ndio wanaohudhuria kliniki wakiongozana na wenza wao kwa ajili ya kupima virusi vya ugonjwa huo hali inayoonyesha kuwa jamii inahitaji msukumo katika hili.

“Natumia fursa hii kuwaomba waheshimiwa madiwani watusaidie kuhamasisha wananchi wote kupima virusi vya ukimwi kwa hiari kwa kuwa sasa hivi mtazamo ni afya chanya na kinga kwa sababu huduma za dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo zinapatikana kwa urahisi kwenye vituo vya afya,” alisema Dk. Mahita.

0 Responses to “ MATANGAZO YA WAGANGA WANAOTIBU UKIMWI YAWAVUNJA MOYO WATAFITI ”

Post a Comment

More to Read