Friday, June 6, 2014
WARIOBA AZISHUKIA UKAWA, CCM.
Do you like this story?
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewashauri
wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CCM kuacha kuzunguka mikoani
kufanya mikutano inayoeleza misimamo yao kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kwa
kuwa haina tija kwa taifa.
Ameonya
kuwa mikutano hiyo inajenga mwelekeo mbaya kwa taifa na kuhatarisha mchakato wa
Katiba na kuzitaka pande hizo kumaliza tofauti zao.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Warioba alisema:
“Kwa mustakabali mwema wa taifa, ni muhimu makundi haya ‘ya-resolve’
(yamalize), matatizo yaliyopo kabla ya Agosti, ili Bunge Maalumu la Katiba
likirejea, wote washiriki na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hili
ni kwa masilahi ya taifa.”
Kauli
ya Waziri Mkuu huyo mstaafu ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu, imekuja
huku makundi ya Ukawa linaloundwa na wabunge wengi wa upinzani na viongozi wa
CCM wakiendelea kung’ang’ania misimamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya
iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Wakati
CCM ikipinga mapendekezo ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu uliomo kwenye
Rasimu, Ukawa unaunga mkono mapendekezo hayo.
Aprili
16, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliiongoza Ukawa kutoka ndani ya
Bunge la Katiba baada ya kumaliza kuchangia mjadala huo, kwa madai ya
kutokutendewa haki na CCM katika mambo mbalimbali ikiwamo kupinga mapendekezo
ya upinzani hata yale ya msingi akisema hawawezi kuwa sehemu ya watu
wanaosambaza chuki na kuwa sehemu ya kuibomoa nchi.
Siku
chache baadaye, Ukawa ulianza mikutano nchi nzima kwa kile ulichodai kuwaeleza
wananchi namna CCM inavyotaka kuchakachua maoni yao yaliyokusanywa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Kwa
upande wake, CCM imekuwa ikifanya mikutano kueleza msimamo na sababu za kutaka
kuendelea kwa muundo wa serikali mbili.
Jaji
Warioba alisema makundi hayo yana nafasi ya kumaliza tofauti zao kabla ya Bunge
Maalumu la Katiba kuanza tena vikao vyake, hivyo kuliwezesha taifa kupata
Katiba Mpya.
Alisema
makundi hayo yasipopatana yanaweza kuhatarisha mustakabali wa taifa hata amani
iliyopo.
Alionya
kuwa amani iliyopo nchini ikivurugika kwa sababu yoyote ni vigumu kuirejesha na
kwamba watakaotaabika ni wananchi.
Jaji
Warioba ambaye aliwahi kuongoza Tume ya Rushwa iliyoundwa na Rais wa Awamu ya
Tatu, Benjamin Mkapa, alisema amani ya Tanzania ikivurugika kutokana na makundi
kupingana katika mchakato wa Katiba wanasiasa ndio watakaonyooshewa vidole.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “WARIOBA AZISHUKIA UKAWA, CCM.”
Post a Comment