Sunday, July 6, 2014

MECHI YA KIRAFIKI KATI YA MBEYA CITY VS PRISON WAONYESHANA UBABE.















Utovu wa nidhamu, vurugu na rabsha za hapa na pale zilizosababisha Polisi wa kutuliza ghasia kuingia katikati ya Uwanja ni miongoni mwa matukio yaliyobeba hisia za wapenzi wa soka Jijini Mbeya ambao walitarajia kuona burudani ya kandanda kati ya timu zenye mashabiki wengi Mbeya City na Prison za Jijini hapa.

Mchezo huo umezikutanisha timu hizo ikiwa ni takribani miezi  mitatu tangu kumalizika kwa ligi hiyo mwezi Aprili mwaka huu huku Prison ikikumbuka majeraha ya kufungwa na Mbeya City bao 1-0 katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Wakicheza kwa kujiamini na kutarajia kushinda mechi hiyo  timu ya Mbeya City  walianza kuonesha utovu wa nidhamu pale mchezaji wa timu hiyo Richard Peter alipofanikiwa kutingisha nyavu za Prison katika dakika ya 25 ilhali mshika kibendera wa kulia mirambo Shikungu akiwa amenyoosha kibendera kuashiria kuwa mchezaji huyo alikuwa ameotea.

Hali hiyo ilianzisha lawama dhidi ya mshika kibendera huyo na kusababisha Mbeya  kutoelewana vyema  ilhali wenzao wa Prison wakijitahidi kutumia fursa hiyo kuonesha kiwango kizuri cha kandanda.

Kwa takribani dakika 14 mchezo huo ulikuwa ni wa kuviziana kati ya Mbeya City na Prison ambapo kunako dakika ya 44 ya mchezo Winga wa kulia wa MBEYA City Deus Kaseke aliambaa ambaa na mpira kuelekea katika lango la Prison.
Kaseke alitoa pasi iliyomkuta Paul Nonga ambaye alipiga shuti lililombabatiza kipa wa Prison Mohamed Yusuf ambaye bila tahadhari aliondosha hatari kwa miguu na kumbabatiza mlinzi wa timu yake Lugano Mwangama na kujifunga goli, dakika ya 44.
Hadi mapumziko Mbeya City walitoka kifua mbele wakiongoza goli 1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko ambapo Prison walizalimika kucheza nusu baada ya mchezaji wao Jeremiah Juma kuzawadiwa kadi mbili za njano kwa mchezo mbaya na kulazimika kutoka nje ya uwanja.

Awali Prison walipata penati iliyolalamikiwa na wachezaji wa Mbeya City ambapo mchezaji wao Deogratius Julius aliunawa mpira eneo la adhabu na kusababisha wachezaji wa timu hiyo kumzonga mshika kibendera lakini hata hivyo penati hiyo iliyopigwa na Ibrahimu Mamba ilipaa juu ya mwamba.

Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mechi hiyo kumalizika huku wachezaji wa Mbeya City wakiamini kuwa wameshinda mechi hiyo, wachezaji wa Prison walilisakama lango la Mbeya City kama nyuki na kusababisha goli lililofungwa kwa kichwa na Frank William.

Kipenga cha kumaliza mpira huo kilichopulizwa na mwamuzi wa kati Kayombo kilisababisha kundi la wachezaji wa timu hiyo kuvamia uwanja na kumzonga mshika kibendera Shikungu ambapo waamuzi wengine waliingilia kati kuzuia tafrani hiyo.
Hali hiyo ilisababisha askari polisi kuingilia kati na kulazimika kuwatoa nje ya uwanja waamuzi wakiwa chini ya ulinzi mkali.

0 Responses to “MECHI YA KIRAFIKI KATI YA MBEYA CITY VS PRISON WAONYESHANA UBABE.”

Post a Comment

More to Read