Monday, July 14, 2014

POLISI WATUMIA MABOMU KUNUSURU WENZAO WASIUAWE.



POLISI Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma walilazimika kutumia Mabomu na risasi za moto kwa wingi ili kuwanusuru Askari wake wawili wasiuwawe katika mzozo uliotokea July 11 mwaka huu kati yao na Wananchi wa Vijiji vya Lukumbule na Mchesi.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa mkasa huo ulitokea katika Kitongoji cha Silaju kilichopo katika Kijiji cha Mchesi huku chanzo cha Mzozo huo kikidaiwa kusababishwa na Polisi hao, baada ya kumzuwia mwendesha pikipiki aliyetambulika kwa Jina la Sijaona Alli (Feruzi) (31) kwa  lengo la kumtaka asimame iliawapatie chochote (rushwa) kama ilivyozoeleka na Polisi wa jeshi hilo hapa nchini.

Sambamba na uharibifu huo pia Wananchi hao waliwajeruhi Polisi wawili baada ya kuwashambulia kwa kuwapiga kwa mawe zikiwa ni juhudi za Wananchi hao kupinga vitendo vya uonevu wa polisi hao ambao waliwatuhumu kuwanyanyasa kila siku kwa kukamata na kuwatoza fedha waendesha pikipiki na baiskeli Kijijini hapo.


Kufuatia vurugu hizo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ililazimika kuongeza vikosi vya polisi katika eneo la kijiji hicho ili
kuwanusuru Vijana hao waliotajwa kwa majina ya namba ,G1921 PC. Chale na H,9239 Pc Benjamini.

Wakisimulia mkasa huo baadhi ya mashuda wa tukio hilo walidai kuwa baada ya Polisi hao kumzuwia mwendesha pikipiki huyo asipite huku akiwa katika mwendo kasi aliwagonga na kuwaumiza vibaya hali ambayo iliyopelekea Wananchi wa Vijiji vya Lukumbule na Mchesi Kuchukizwa na kitendo hicho baada ya kukitafsiri na kuamini kuwa ni Uonevu.



Wakiongea kwa nyakati tofauti Diwani wa kata ya Lukumbule Bw Issa Kitumbi na watendaji wa Vijiji vya Mchesi Bw Ali Mnandi na Omari Chowo wa Lukumbule walisema kuwa vurugu zilianza kujitokeza katika Zahanati ya kata hiyo baada ya Wananchi kupeana taarifa juu ya tukio hilo hali ambayo ilimfanya muuguzi wa kituo hicho kuwafungia ndani Polisi na majeruhi hao na kupiga simu kituo kikuu cha polisi Tunduru ili kuomba msaada wa kuwanusuru polisi wasishambuliwe na Wananchi hao.


Akiongea kwa taabu majeruhi Sijaona Alli (Feruzi) ambaye amelazwa kitanda namba 16 katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru kwa matibabu alisema kuwa alikumbwa na mkasa huo wakati akirejea kutoka shambani ambako alienda kupulizia mikorosho yake na kwamba alisimamishwa ghafla katika eneo la kona.


Aliendelea kueleza kuwa wakati akijaribu kupunguza mwendo kwa kurudisha gia ili asimame ghafla pikipiki yake namba T823 Cfr
ilipigwa teke na askari aliyemtaja kwa jila moja la PC Benjamini na kujikuta anaanguka na kuumia.


“Nilikuwa natoka shambani kupulizia mikorosho yangu ghafla nikasimamishwa eneo la kona iliyopo katika Mtaa wa Silaju, lakini wakati najiandaa kusimama pikipiki yangu ilipigwa teke na kunifanya nikose balansi na kuangua” alisema Feruzi.


Feruzi aliendelea kueleza kuwa kutokana na yeye kuwa na mahusiano mazuri na baadhi ya polisi katika kituo hicho amekuwa akisimama na kuzungumza nao kila anapo simamishwa nao na akaongeza kuwa wiki moja iliyopita polisi hao walimkamata na kumtoza faini ya shilingi 60,000/= kisha kumpatia kibali cha kutomkamata tena hali ambayo ilimfanya aonekane kutokuwa na uhasama wala mashaka nao tena.


Akizungumzia mkasa huo Kaka wa majeruhi huyo Bw. Said Alli aliwaomba Viongozi wa jeshi hilo kumsaidia ndugu yake kwa kutenda haki, kwani Polisi wa ngazi ya chini wameanza kumtishia ndugu yake kuwa watamkata miguu.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Bw.  Msikhela Mihayo amethibitishakuwepo kwa tukio hilo la mapigano kati ya Polisi na Wananchi hao pia walichoma moto pikipiki yenye namba za usajili T 342 CEX aina ya SNLG
ambayo mali ya askari polisi No,H 925 PC Benjamini,mtambo wa kufulia umeme jua (SORLA),Madirisha mawili,Televisheni pamoja na kung’oa paa la kituo hicho.

Kamanda Msikhela aliendelea kufafanua kuwa kufuatia tukio hilo mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa licha ya kuwa kikosi maalumu cha polisi toka polisi mkoa ambacho kinaongozwa na afisa upelelezi wa makosa ya jinai ya mkoa Bw. Revokatus Malimi kimeshapelekwa na kinaendelea kuwasaka watuhumiwa ili sheria iweze kufuata mkondo wake .

Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa kamati ya mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho pamoja na kukiri kuwepo kwaa tukio hilo alieleza kuwa hali kwa hivi sasa katika kijiji hicho ni shwari na hivi sasa wapo kwenye kikao cha Ulinzi na usalama kufanya tathimini ya hasara iliyotokea.

Na Steven Augustino wa demashonews, Tunduru

0 Responses to “POLISI WATUMIA MABOMU KUNUSURU WENZAO WASIUAWE.”

Post a Comment

More to Read