Tuesday, July 15, 2014

PRISONS YAIONYA MBEYA CITY.


Tanzania prisons

Mbeya City Fc

Mbeya. Timu ya Tanzania Prisons imeapa kuondoa uteja kutoka kwa Mbeya City msimu ujao na kusisitiza kwamba vijana wa timu hiyo wanajinoa kisawasawa kuondokana na hali hiyo.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shaban Kazumba, ambaye amejiunga na timu hiyo hivi karibuni, alisema pamoja na msimu uliopita Mbeya City kuifunga Prisons mechi zote mbili, msimu ujao mambo yatabadilika na kuitaka Mbeya City kutambua hilo.

Kazumba alisema kwa sasa timu ina vijana wadogo ambao imewapandisha daraja kutoka timu B, na kusajili wengine wawili waliokuwa huru kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na kwamba inafanya mazoezi katika Uwanja wa Sokoine kila siku.

“Tumeamua kuwapandisha daraja kutoka U-20 kuja kuitumikia timu yetu kwa msimu ujao kwa sababu tumeona wamekuwa na uwezo wa kupambana pindi wawapo uwanjani, lakini pia tumesajili wachezaji wawili waliokuwa huru na sasa wataichezea timu yetu kwa mkataba,” alisema Kazumba.

Wachezaji waliopandishwa daraja ni pamoja na kipa Beno
Kakolanya, Mfaume Omary, Frank William, Said Mtupa, Jacob Mwakalobo na Lambary Sybianka.Alisema wachezaji waliokuwa huru na sasa wamesajiliwa na timu hiyo ni pamoja na James Josephat na Meshack Olest, na kwamba Tanzania Prisons ina jumla ya wachezaji 28 na sasa dirisha la usajili wa awali limefungwa.

Hiyo ni moja ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo sasa imesogezwa mbele siku ya kuanza.
Awali michuano hiyo ilikuwa ianze Agosti 24, lakini sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameisogeza mbele na itaanza Septemba 20.

Sababu za mbalimbali zilitajwa na TFF katika uamuzi huo, ambapo pia ni kupisha michuano ya Kombe la Kagame.

0 Responses to “PRISONS YAIONYA MBEYA CITY.”

Post a Comment

More to Read