Monday, July 14, 2014

SIMBA YASHUSHA WAWILI KWA MKUPUO.



SIMBA inamaliza mazoezi ya gym leo Jumatatu na kuanzia jioni itageukia mazoezi ya uwanjani kwa siku saba kabla ya kwenda Zanzibar kupiga kambi ukiwa ni mkao wa Ligi Kuu na Maadhimisho ya Simba Day Agosti 8.

Lakini jioni ya leo itashusha kwenye uwanja wa Chuo Kikuu wachezaji wawili wapya, mshambuliaji Michael Mgimwa na Jabiri Aziz ‘Stima’ huku ikiendelea kumalizana na wengine.

Mgimwa ni mchezaji aliyelelewa na kituo cha TFF na baadaye alienda kucheza Thailand wakati Stima ni mchezaji huru baada ya kutemwa na Azam FC. “Tuna nafasi mbili za wachezaji wa kigeni na mbili wachezaji wazawa, hao watafanya mazoezi na Simba ili kocha aone viwango vyao maana hatuwezi kusajili bila kujua mchezaji ana kiwango gani na hatuwezi kusema moja kwa moja kama watachukuliwa ama wataachwa mpaka kocha aridhike,” alisema Said Tuliy ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Usajili.
Simba Ijumaa ilitangaza kumaliza usajili wake ndani ya saa 48 kwa maana ya hadi kufikia jana Jumapili, lakini ikashindikana kutokana na wachezaji wao wengi kudai dau kubwa ambalo haliendani na thamani zao. Vile vile kocha ametaka kuwaona mazoezini kabla ya kuwasainisha.

Habari kutoka ndani ya Kamati ya Mashindano zinasema kwamba baada ya mechi ya Simba Day itakayochezwa jijini Dar es Salaam, kikosi kitakwenda kuweka kambi yake nje ya nchi ambapo mpaka sasa bado wapo katika mchakato wa wapi wakaweke kambi hiyo ingawa kuna mapendekezo ya kwenda Oman.

“Tunataka Simba ifanye vizuri msimu ujao ndiyo maana yote haya yanatakiwa kufanywa mapema ili tusiwe na maandalizi ya zima moto, ni kwa sababu tunataka kuwa na msimu bora,” aliongeza kiongozi huyo.

“Tunasubiri watu wa Kamati ya Usajili wamalize kazi yao ya kusajili ili tutakapokwenda Zanzibar kikosi kiwe kimekamilika, ndiyo maana mazoezi yetu ya hapa yanachukuwa kama siku saba na tutakwenda Zanzibar kwa kambi ya awali ya maandalizi ya Simba Day.”

Kuhusu wachezaji wao wa kigeni mabeki Joseph Owino na Donald Mosoti, alisema: “Owino anaingia Jumatano (keshokutwa) lakini Mosoti bado haijafahamika kwani mawasiliano ni magumu ingawa tunasikia yupo Uarabuni.”

0 Responses to “SIMBA YASHUSHA WAWILI KWA MKUPUO.”

Post a Comment

More to Read