Wednesday, August 27, 2014

0 HIZI HAPA MBINU 14 ZITAKAZOKUSAIDIA KUJIAMINI KATIKA MAISHA YAKO.




Kila kitu ambacho ni halisi kinawezekana. Bila shaka unakumbuka vizuri kuhusu namna kutojiamini kwetu kunavyojengwa. Kwa kuwa tunajua chanzo, ni rahisi kupata tiba.


Njia zifuatazo zinaweza kukusaidia katika kujenga kujiamini. Kuna njia nyingi zinazopendekezwa, lakini kuna zile ambazo zimetumika sana katika kufanya kazi hiyo. Hizi zifuatazo ni baadhi yake.

1. Yachunguze mawazo yako na vitendo vyako kwa uangalifu ili kujua ni kitu gani hukufanya usisimke. Anza kufanya mambo ambayo unaona kwamba una uwezo kuyafanya bila wasiwasi na kuchukua uamuzi unaojitegemea kufuatana na utashi wako. Ikibidi unaweza kuomba msaada wa wengine, lakini jaribu kila mara kufanya mambo kufuatana na unavyoyaona.

2. Jifunze kujithamini. inawezekana kwa miaka na miaka umekuwa unajiona kama mtu usiye na thamani. Pia unaweza ukaona kwamba, hadhi uliyokuwa nayo mbele ya ndugu, jumuiya na jamii imepungua. Jali ujuzi na vipaji vyako; hata kama kuna ndugu wametajirika pamoja na kuwa ni mbumbumbu hiyo isiwe chanzo cha kukuvunja nguvu. Iko siku utafanikiwa kama utaanza kujiamini.



3. Jisamehe bila masharti yoyote. Kama maisha yako ya awali yalikuwa si ya kiungwana, jisamehe na anza maisha yako upya. Njia bora ya kujisamehe ni kujipenda bila masharti yoyote.

4. Pambana na hofu. Hofu ni kitu kibaya sana kwa sababu inaingilia kwenye uwezo wako wa kufikiri. Ili ufanikishe malengo yako ya maisha huna budi kuhakikisha kuwa huna hofu tena.

5. Fanya vitu unavyoviogopa. Orodhesha idadi ya vitu ambavyo ulikuwa unaviogopa. Kisha anza na vitu ambavyo unaviogopa zaidi na jiulize kwa nini usiweze kuvifanya.

6. Jifunze kupambana na kushindwa. Kubali kwamba kushindwa ni kama chombo cha kujifunzia na si kitu cha kukukatisha tamaa. Jua, na amini kwamba, bila kushindwa hakuna kukua. Pia elewa kwamba, kushindwa siyo dalili ya udhaifu, bali uimara.



7. Kubali kupingwa kwa moyo mkunjufu. Watu wa nje wanaweza kukusaidia kwa mambo yako mengi ambayo huyaoni. Watu wakikusoa, hata kama ni kifedhuli, chukua yaliyo mema na yafanyie kazi.

8. Fanya mazoezi ya kujiamini. Jifunze kusimama kwa miguu yako mwenyewe kimawazo, kiimani na kimatendo. Bila kuonyesha ujeuri unaweza kulinda haki zako, matarajio yako na maadili yako. Anza kujifunza kujenga taswira ya kujiona uko mwenyewe na unamudu kila kitu. Bila msaada na utegemezi kwa wengine.

9. Jipongeze kwa maneno mazuri. Jiamini na daima jipe moyo kwa maneno ambayo yatakutia moyo ili kwenda vyema katika shughuli zako. Usitumia maneno ya kejeli, kashfa na chuki dhidi yako mwenyewe, ‘mimi ni mjinga kweli yaani jambo dogo kama hili limenishinda….’ Unaweza kujisemea baada ya kukosea. Kama umekosea, jiambie maneno mazuri ya kujipa moyo na siyo maneno ya kero na fadhaa.

10. Usijilinganishe na wengine, bali iga. Kama wengine wanakuzidi isikukatishe tamaa ila iwe ni chachu ya maendeleo . jiambie, ‘kama wanaweza, maana yake ni kwamba, inawezekana, nami nitaweza tu.’

11. Fikiria mambo ambayo yanakufanya usiwe na furaha na jaribu kupambana nayo na kuondokana nayo. Kila wakati jiulize, ni kwa nini uko kwenye hali ya kihisia uliyo nayo. Usikubali kufuga huzuni kwa muda mrefu ndani mwako.



12. Fanya mambo uyapendayo zaidi. Kujiamini kutaongezeka kama utafanya mambo unayoyafahamu zaidi kwa sababu ni rahisi kuyafanikisha na kukuletea furaha.

13. Jifunze namna ya kushughulikia hasira zako. Mtu asiyejiamini ana kawaida ya kutaka kupendwa na watu, na katika kufanya hivyo, hapendi kuonekana kuwa ni mtu mwenye hasira na hivyo kuendelea kubakia na hasira zake moyoni hata kama ameudhiwa.

14. Kuzuia hasira hakusaidii, zaidi ya kukuongezea kuchanganyikiwa na kukufanya kuwa mtu usiye na furaha au kisirani. Ukiudhiwa, mwambie aliyekuudhi kinaganaga, lakini katika mazingira ya kistaarabu ambayo hayawezi kukuumiza wewe wala mtu ambaye amekuudhi.

0 Responses to “0 HIZI HAPA MBINU 14 ZITAKAZOKUSAIDIA KUJIAMINI KATIKA MAISHA YAKO.”

Post a Comment

More to Read