Tuesday, September 16, 2014

BABA AWAFUNGIA WATOTO NDANI MIEZI 10, WASHINDIA MLO MMOJA, MTOTO MMOJA AFA.




Mwanaume mmoja mkazi wa Kijiji cha Msimba wilayani Uvinza, Kigoma, anashikiliwa na Polisi akidaiwa kufungia watoto wake wanne ndani ya nyumba na kuwashindisha njaa kwa takribani miezi 10.

Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, iliwabaini watoto hao hivi karibuni kijijini Sunuka, wilayani Uvinza. Kati yao, watatu ni wa kiume.

Mkubwa ana umri wa miaka minane akifuatiwa na msichana mwenye umri wa miaka saba. Wengine wana umri wa miaka sita na minne.

Hayo yalithibitishwa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Penina Mbwete alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kumtaja baba mzazi wa watoto hao kuwa ni Mateso Hassan (35).

Tayari baba huyo anashikiliwa na Polisi ambapo awali ilikuwa katika Kituo cha Ilagala kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma wakati akisubiri kupandishwa kizimbani kusomewa tuhuma za kudaiwa kuwafungia watoto hao na kuwazuia kwenda shule huku wakipata mlo mmoja tu, tena usiku wa manane.

Mjomba wa watoto hao, Sunday Zuberi (38) alidai mama mzazi wa watoto, Yauzia Zuberi (38) alipigwa na mumewe na kuamua kukimbia akiwa na mtoto mwingine mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja, ambaye pia alifariki baada kuugua na kukosa matibabu sahihi.

Alisema kwa kushirikiana na ndugu wengine na baadhi ya wanakijiji cha Msimba, walifanya mpango wa kuwaokoa watoto hao na kumkamata baba yao.

Alidai katika maisha yao ya ndoa, mama wa watoto hao alizuiwa kuhudhuria kliniki wakati akiwa mjamzito hivyo watoto wake wote watano alilazimika kujifungulia kwa wakunga wa jadi .

“Watoto wote hawakuwahi kutibiwa hospitali kwani baba yao alitaka watibiwe kwa dawa za kienyeji,” alidai Sunday.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii Mbwete, watoto hao (majina tunayahifadhi) wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni kwa uchunguzi wa kitabibu.

  “Nitakachokifanya ni kuhakikisha kuwa baada ya tiba watoto hawa wanakuwa katika mikono salama. Natoa rai kwa ndugu yeyote ambaye ana uwezo, kukaa nao, lakini wawe salama…baada ya hapo tutakuwa tukiwatembelea kuhakikisha kuwa kweli wanaendelea kuwa salama.” alisisitiza Mbwete.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Makris Yakayashi alisema baada ya uchunguzi wa kitabibu, imebainika watoto hao wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa damu, utapia mlo mkali na matatizo mengine ya kisaikolojia na upungufu wa kinga unatokana na kutopata lishe ya uhakika.

Mama mzazi wa watoto hao, Gauzia Zuberi alisema katika maisha yao ya ndoa, mumewe alikuwa akiwatesa kwa kuwapiga, kuwanyima chakula na wakati mwingine kuwamwagia maji akidai anawaogesha kisha kuwatembeza mtaani usiku kucha.

Credit: Habari leo

0 Responses to “BABA AWAFUNGIA WATOTO NDANI MIEZI 10, WASHINDIA MLO MMOJA, MTOTO MMOJA AFA.”

Post a Comment

More to Read