Thursday, September 18, 2014
MAPACHA WALIOUNGANA MWILI WILAYANI MAKETE MKOANI NJOMBE KUHITIMU KIDATO CHA NNE MWAKA HUU.
Do you like this story?
Hatua ya kwanza ya
ndoto ya kuzama katika elimu ya mabinti pacha walioungana kiwiliwili, Consolata
na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoa mpya wa
Njombe, inatarajiwa kutimia Novemba mwaka huu, wakati mabinti hao watakapofanya
mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.
Itakumbukwa kwamba
walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao Ikonda, walikuwa
na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema wanataka kuwa
wasomi waliobobea katika utaalamu wa kompyuta. Lakini, kwa sasa, wanasema
wanatamani kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi.
Wanafunzi hao mwaka
2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar
es Salaam.
Kwa sasa wanasoma
katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo
mkoani Iringa.
Shule hiyo
inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari Wakatoliki wa Italia,
kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Wakizungumza na
mwandishi wa habari hii shuleni hapo hivi karibuni, walisema wanafurahi kuwa
miongoni mwa watahiniwa watakaofanya mtihani huo wa kidato cha nne mwaka huu.
"Tunafurahi, tunajiandaa tunasoma
kwa bidii, mtihani uko karibu tunataka tufaulu vizuri masomo yetu, ili ile
ndoto yetu ya kuwa Makatibu Muhtasi itimie," walisema Maria na Consolata, ambao
wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani, ambako pia wana kiti maalumu.
Pacha hao
wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana madaftari
yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza
kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
"Wala hatupati shida tumezoea,
kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria
anaandika kwa mkono wa kulia,"
anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Shule hiyo ina
wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Ilianzishwa mwaka 2006 na hivi
sasa ina jumla ya wanafunzi 183. Wote wanaishi kituoni hapo na wote wanatoka
kwenye mazingira magumu.
Changamoto kubwa
iliyokuwa shuleni hapo ni ukosefu wa nishati ya umeme, ambapo uongozi wa shule
na kituo hicho unalazimika kutumia jenereta na umemejua, jambo ambalo mapema
wiki hii Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa
kuwapelekea umeme.
Pacha hao walizaliwa
mwaka 1996 wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani
Iringa.
Walifaulu mtihani wa
darasa la saba mwaka 2010, ambapo kila mmoja alipata alama 151, ingawa
walitofautiana ufaulu kwenye masomo yao.
Katika somo la
Maarifa ya Jamii, Consolata alipata alama 29 na Maria alama 25, kwenye somo la
Kiingereza, Maria alipata alama 36 na kumzidi Consolata aliyepata alama 34,
wakati kwenye somo la Sayansi, Maria alimzidi Consolata kwa kupata alama 31
dhidi ya 29.
Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi iliwapanga pacha hao kujiunga na kidato cha kwanza katika
Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo
hawakujiunga na sekondari hiyo, kutokana na hali yao na pia umbali kutoka
Iringa hadi Dar es Salaam. Ndipo Wamisionari hao wakawachukua mwaka 2011 na
kuanza kidato cha kwanza.
Walizaliwa kwenye
Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996. Lakini, taarifa zao hazikufahamika
hadi pale walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda na kutafutiwa mlezi wa
kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa bado wadogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAPACHA WALIOUNGANA MWILI WILAYANI MAKETE MKOANI NJOMBE KUHITIMU KIDATO CHA NNE MWAKA HUU.”
Post a Comment