Thursday, September 18, 2014
MTUHUMIWA KESI YA UGAIDI AWALALAMIKIA POLISI KWA KUMMINYA SEHEMU ZAKE ZA SIRI NA KUMCHOMEKA MTI SEHEMU ZA HAJA KUBWA
Do you like this story?
Mtuhumiwa katika kesi
ya ugaidi, Abdallah Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,
kumruhusu kutohudhuria siku za kesi na abaki magereza, kutokana na maumivu makali
anayodai anayapata sehemu za siri alikominywa na polisi na kuingiziwa mti
kwenye haja kubwa.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako
inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata
maumivu makali sana sehemu za siri kunauma kwa sababu polisi walinitesa kwa
kuniingizia mti kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,” alisema.
Alisema mbele ya
Wakili wa Serikali, Rose Sulle kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri, pia
mguu wake uliokatwa hospitalini, bado unamsumbua kutokana na maumivu.
Maginga pia aliomba
iagize Magereza wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata
matibabu Septemba 5 mwaka huu, ila alizuiwa hadi sasa.
Akijibu hoja hizo,
Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devotha Msofe, alisema suala la kuja
mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia, alimshauri
mshitakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi, amweleze hakimu anayesikiliza kesi
yake, Mustapher Siyani ambaye kwa siku hiyo hakuwepo.
“Sikiliza Maginga suala la kuja
mahakamani ni lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila kuhusu kwenda
hospitalini liwasilishe Magereza ndio mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema.
Awali ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo
chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi, ambapo Sheria Namba 22 ya Mwaka 2002
inasema upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya
kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washitakiwa hao
wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha
vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka
hayo, pia wanahusishwa na tukio la mlipuko wa bomu lilitokea baa
ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na
kujeruhi wengine 16.
Watuhumiwa wengine
wanaokabiliwa na mashitaka hayo ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti, Ally
Hamisi, Abdallah Wambura, Rajab Hemedi, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yassin
Sanga, Shaaban Wawa, Swaleh Hamisi, Abdallah Yassin, Abdallah Maginga na Sudi
Nassib Lusuma.
Wengine walioongezwa
katika shauri hilo ni Shaaban Mussa, Athuman Hussein, Mohammed Nuru, Jafari
Lema, Abdul Mohammed na Said Michael Temba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MTUHUMIWA KESI YA UGAIDI AWALALAMIKIA POLISI KWA KUMMINYA SEHEMU ZAKE ZA SIRI NA KUMCHOMEKA MTI SEHEMU ZA HAJA KUBWA”
Post a Comment