Tuesday, September 2, 2014

PINDUAPINDUA YA RASMU YA KATIBA




Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba linaanza vikao vyake tena leo mjini Dodoma, huku kukiwa na jitihada kubwa za kujaribu kuweka udhibiti wa mjadala utakavyoendeshwa miongoni mwa wabunge, wengi wao wakiwa ni kutoka chama tawala CCM.

Kuna hofu ndani ya chama hicho kwamba mgawanyiko uliojitokeza wakati wa vikao vya kamati utahamia kwenye Bunge zima ambako mbali na waandishi wa habari kuruhusiwa kushiriki, pia huonyeshwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni.

Msigano unaotabiriwa kutokea ni ule uliojengwa katika mambo yaliyozua mvutano ndani ya kamati kiasi cha wajumbe wenye itikadi moja kusigana kwa misingi tofauti lakini kubwa likiwa ni lile la Uzanzibari na Ubara.

Tofauti hizo za kimaeneo zilionekana dhahiri wakati wa mjadala wa Sura ya Tisa na 10 ambazo zinahusu muundo wa Bunge na mambo mengine ya utawala, pia katika Sura ya 14 hususan mgawanyo wa mapato.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo walitabiri mvutano mkali bungeni, wakirejea hali ilivyokuwa ndani ya kamati zao ambako baadhi ya wajumbe hawakuridhika na baadhi ya uamuzi.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Nne, Christopher Ole Sendeka alisema mjadala katika kamati yake ulikuwa mkali na kwamba hali itakuwa ni ngumu zaidi watakapoingia bungeni.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael alisema suala la ardhi linaweza kuzua mvutano mkali kwani ni moja ya mambo muhimu katika Katiba.

Makamu Mwenyekiti wa kamati Namba Kumi na Moja, Hamadi Yusufu Masauni alisema jambo pekee analotarajia kuwa litasumbua ni muundo wa Bunge la Muungano.
Alisema unapotajwa muundo wa Bunge ndipo unapotajwa mfumo wa Muungano ambao umekuwa ni kero ya muda mrefu.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu alisema hofu yake iko kwenye suala la mgawanyo wa mapato ambalo kamati yake ilisita kulijadili hadi walipoitwa wataalamu kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Fedha za Muungano na ile ya Zanzibar.

Kwa msingi huo, wakati kamati zikianza safari ya siku tano kuwasilisha taarifa zake kuanzia leo hadi Septemba 8, mwaka huu, kutakuwa na maoni ya wachache katika baadhi ya kamati suala ambalo linatoa picha ya kuwapo kwa mawazo tofauti katika mambo kadhaa.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mengi ya mambo hayo ni yale yaliyobadilishwa kinyume na yalivyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyotungwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au mambo mapya yaliyoingizwa kwenye rasimu hiyo.

0 Responses to “PINDUAPINDUA YA RASMU YA KATIBA”

Post a Comment

More to Read