Friday, September 19, 2014
POLISI WATEMBEZA KICHAPO KWA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DAR.
Do you like this story?
MUENDELEZO wa Jeshi
la Polisi nchini kuwanyanyasa, kuwatisha waandishi wa habari na kuwafanya
wasitekeleze wajibu wao ipasavyo, ilijidhihirisha wazi jana makao makuu ya
jeshi hilo, baada ya waandishi kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue
taarifa za kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe.
Tukio la kupigwa na
kudhalilishwa kwa waandishi wa habari lilitokea jana, limetokea ikiwa ni siku
moja baada ya Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya
ulinzi na usalama nchini kushirikiana na waandishi wa habari katika kufanya
kazi kwa ajili ya kulinda amani ya nchi.
Waandishi waliyopigwa
na Polisi hiyo jana ni Josephat Isango anayeandikia gazeti hili, huku Yusuph
Badi ambaye ni mpiga picha wa magazeti ya serikali, akipigwa na ‘kusakiziwa’
mbwa ili wamuume.
Dalili za waandishi
wa habari kuzuiwa kufanya kazi yao, zilianza kujionesha mapema jana wakati
Mbowe alipowasili katika makao makuu ya Jeshi la Polisi, ambako waandishi
walizuiwa wasiingie katika eneo hilo kwa ajili ya kuchukua picha na maelezo ya
kiongozi huyo.
Akiwa anawaongoza
askari wake katika amri ya kushambuliwa kwa waandishi wa habari hiyo jana,
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisikika mara kwa mara
akiwaagiza vijana wake wawaondoe waandishi na hata kuwasakizia mbwa.
Chagonja, alisikika
mara kadhaa akitoa amri kwa askari kuwa wawafungulie mbwa ili waweze kujeruhi
angalau mtu mmoja kutoa funzo ili wafuasi wa CHADEMA waliokuwa kwenye lango
kumsubiri Mbowe waondoke.
“Waondoeni wote
msiwaruhusu hata hao waandishi kuingia humu, ninyi askari wa mbwa mnafanya nini
hapo wakati watu wamejazana mlangoni wapelekeeni hao,” alisikika akisema
Kamishna Chagonja.
Mara baada ya
maelekezo hayo ya Kamishna Chagonja, askari waliokuwa na mbwa walianza
kuwakimbiza wafuasi wa CHADEMA na waandishi wa habari.
Katika hali ya
kustaajabisha, askari watatu kwa pamoja walimfuata Josephat Isango, aliyekuwa
akitoka katika lango kuu na kuanza kumshambulia kwa rungu na mateke hali
iliyowafanya waandishi wa habari kuingilia kati kwa ajili ya kumnusuru.
Baada ya waandishi
kumnusuru Isango, kipigo kiligeukia kwa Mwandishi Yusuph Badi, ambaye wakati
akishambuliwa alianguka chini huku askari wenye mbwa wakiwaachia kwa ajili ya
kumshambulia.
Kilichomnusuru Badi
asiumwe na mbwa hao ni kamera aliyoishika mkononi na kujikinga ili asidhurike,
kitendo hicho cha kujikinga kilisababisha kuharibika kwa kifaa hicho.
Wakizungumza baada ya
hali kutulia, Badi na Isango, walieleza kuwa kilichofanywa na jeshi la Polisi
ni kuminya uhuru wa utendaji kazi wa waandishi katika kuuhabarisha umma wa
watanzania juu ya mambo yaliyokuwa yakitokea.
“Ni jana tu
wameambiwa namna ya kutoa ushirikiano na vyombo vya habari, lakini leo
wanatupiga na kutusakizia mbwa hii si haki na viongozi wetu wanapaswa waangalie
mara mbili mbili namna ya kushirikiana na jeshi hili,” alisema Badi.
Jeshi la Polisi
limekuwa na kawaida ya kuwanyanyasa, kuwapiga na hata kuwaua waandishi wa
habari pale wanapotekeleza wajibu wao wa kukusanya habari.
Tukio linalokumbukwa
zaidi la ukatili wa askari wa jeshi hilo kwa waandishi wa habari ni mauaji ya
Mwandishi wa kituo cha Televisheni ya Chanel ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi,
mauaji yaliyotokea Septemba 2 mwaka juzi katika Kijiji cha Nyololo Mufindi
mkoani Iringa wakati mwandishi huyo akiwajibika kukusanya habari.
CHANZO:TANZANIA
DAIMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “POLISI WATEMBEZA KICHAPO KWA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DAR.”
Post a Comment