Tuesday, October 7, 2014
MWANAFUNZI AMTUNDIKA MIMBA MWALIMU WAKE HUKO RUKWA,WAZAZI WATOA MACHO.
Do you like this story?
WAKATI
ikiwa imezoeleka kuwa baadhi ya walimu wa kiume huwarubuni wanafunzi wao wa
kike na hata kuwaharibia kabisa ndoto zao za kielimu kutokana na kuwapa
ujauzito, hali imekuwa tofauti mkoani Rukwa ambako mwanafunzi wa Kidato cha
Pili anadaiwa kumzalisha mwalimu wake.
Mwanafunzi huyo
aliyemzalisha mwalimu wake ana umri wa miaka 17, wakati mwalimu huyo
anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya Umma ya Nkasi, iliyopo mwambao mwa
Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa, ana umri wa miaka 25.
Tukio hilo
linalotajwa kuwa la kwanza kutokea wilayani hapa, limekuwa gumzo kubwa kwa
wakazi wa Nkasi na wilaya jirani.
Hata hivyo, kwa
wanafunzi, wamekuwa wakimpongeza mwenzao kwa kujaliwa kupata mtoto katika umri
wake huo mdogo, huku mzazi mwenzake akiwa na uhakika wa maisha kutokana na kuwa
ni mtumishi serikalini.
Imeelezwa kuwa licha
ya tukio hilo, mwalimu huyo aliyezaa na mwanafunzi wake bado anaendelea na
masomo shuleni hapo, huku `mzazi’ huyo wa kiume akifundishwa na mzazi mwenzake.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mjini Namanyere hivi karibuni, Mkuu wa Shule ya
Sekondari Nkasi mjini Namanyere ambayo ni ya mchanganyiko ya umma, Amiamie
Nanga alisema mwalimu huyo alianza kazi shuleni hapo ikiwa ni mara yake ya
kwanza kufundisha baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu chuoni.
“Yameshatokea, lakini haileti picha
nzuri sana, lakini mimi nina uzoefu mkubwa na wakazi wa mwambao wa Ziwa
Tanganyika, kwao si ajabu kuwa na uhusiano na watu waliowazidi umri, iwe kwa
mtoto wa kike au wa kiume, wote ni sawa tu…
“Lakini katika kisa hiki, inaonesha
walimu sasa wanapoteza haiba ya ualimu. Hii kazi ina miiko na maadili yake …kwa
mwalimu huyu hii ni ajira yake ya kwanza, nikimaanisha ni kituo chake cha
kwanza cha kazi tangu ahitimu masomo yake…” alisema.
Akizungumzia tukio
hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema hakuna kosa kwa
mwalimu huyo wa kike kwa kuwa tayari ni mtu mzima.
“Isitoshe katika kisa hiki ni nadra
kumpata mlalamikaji … Mwalimu mwenyewe huyu wa kike hawezi kuwa tayari
kujidhalilisha kuwa amebakwa, yalikuwa maamuzi yake.”
Aliongeza kuwa, kwa
mwalimu huyo kupata ujauzito wa mwanafunzi wake hakuwezi kuathiri ajira yake,
tofauti na mwalimu wa kiume akimpatia ujauzito mwanafunzi wake wa kike ambaye
huathirika kwa kukatisha masomo.
Jitihada za kumpata
mwalimu huyo wa kike na mwanafunzi huyo zimegonga mwamba baada ya watu wao wa
karibu kumweleza mwandishi kuwa hawako tayari kuuzungumzia mkasa
huo.
Baadhi ya wanafunzi
wa shule hiyo waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa masharti ya
kutoandikwa majina yao kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu shuleni
hapo, pamoja na kukiri kutambua uhusiano baina ya mwanafunzi mwenzao na mwalimu
wao, lakini walisema hivi sasa mwalimu huyo amesitisha uhusiano na mwenzao na
kuanzisha uhusiano mpya na mwalimu mwenzao.
Walisema pamoja na
mambo mengine ni kama mwanafunzi mwenzao ameathirika kisaikolojia baada ya
‘kupinduliwa’ na mwalimu wake wa kiume ambaye kwa sasa ndiye baba mlezi wa
mtoto.
“Huyu mwalimu wa kike sisi sasa tunamwita
shemeji yetu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwenzetu… penzi lao lilikolea
hadi sasa ameweza kumzalia mtoto huyo…, lakini kwa sasa inavyoelezwa ni kwamba
penzi limehamia kwa mwalimu mwenzake,“ alisema
mmoja wao.
Baadhi ya watu wa
karibu na mwanafunzi huyo wanakiri kuwa mwanafunzi huyo hana uwezo wa kifedha
kumudu kumpatia malezi stahiki mtoto wake huyo, hivyo hata mzazi mwenzake
alipoanza uhusiano na mwalimu mwenzake hakuwa na jinsi, bali kukubaliana na
matokeo.
“Usiniandike jina, sisi tunashauri
mwalimu huyo wa kike na mpenzi wake huyo wa kiume ambaye ni mwalimu mwenzake
wahamishiwe shule nyingine kwa sababu kama kioo katika jamii wameteleza kwa
kiasi kikubwa na watashindwa kuwajenga na kuwalea wanafunzi wao kimaadili.
“Isitoshe tunajiuliza sheria hapa
inasemaje maana kama angekuwa ni mwalimu wa kiume amempatia mwanafunzi wake wa
kike ujauzito angeshitakiwa na kufikishwa mahakamani na pengine kuhukumiwa
kifungo kisichopungua miaka 30 jela, sasa kwa hili sheria inasemaje?”Alihoji.
Baadhi ya wazazi
mkoani hapo waliohojiwa na mwandishi kwa nyakati tofauti wameelezea kushangazwa
na tukio hilo, na hasa kwa jinsi mwalimu alivyoshindwa kujizuia `kujiachia’
kimapenzi kwa mwanafunzi wake.
via>>Habarileo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “ MWANAFUNZI AMTUNDIKA MIMBA MWALIMU WAKE HUKO RUKWA,WAZAZI WATOA MACHO.”
Post a Comment