Tuesday, September 9, 2014
YANGA YACHEMKA SUALA LA OKWI, UTATA WAISHA.
Do you like this story?
Kamati ya Sheria na
Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana
juzi (Septemba 7 mwaka huu) na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa
kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba huo ulipitiwa
na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga, na
kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika.
Ukiwa ni mkataba wa
pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
Yanga ikiwa mwajiri,
haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27 mwaka huu
ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni
mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote.
Mkataba ni uhusiano
kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati imebaini kuwa
uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea
kufanya kazi pamoja.
Pamoja na Yanga
kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa sababu za
kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa kilichopo mbele ya
kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili.
Pia lilijitokeza
suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri. Kamati imeiagiza
Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea taarifa katika
kikao kijacho.
Hata hivyo mjumbe
huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi. Uamuzi wa kamati
ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura.
Kuhusu pingamizi la
Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu hiyo imevunja mkataba
kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara wa miezi
mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal
Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na
mwanasheria wake.
Vilevile Kamati
imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA)
kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika mkoa wake bila kulipiwa
ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa kulipa ada hizo.
Pia Kamati imeagiza
klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia uhamisho, kulipa ada za
uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi, vinginevyo leseni zao zitazuiwa
hadi watakapolipa.
Mashauri mengine ya
pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya
kufika mbele ya kamati.
Kamati inasisitiza
kwa wanachama wa TFF kuheshimu mikataba.
BONIFACE WAMBURA
KAIMU KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA
WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “YANGA YACHEMKA SUALA LA OKWI, UTATA WAISHA.”
Post a Comment