Tuesday, September 9, 2014

DALADALA IRINGA ZANYWEA ZASITISHA MGOMO ZENYEWE WANANCHI WATISHIA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI ......



Wanafunzi pamoja na watu mbalimbali wakiwa stand wakisubiri daladala siku ya jana


PAMOJA   na  madereva  wa daladala  mjini  Iringa  jana  kutangaza  kuwa mgomo  wao  ulioanza jana hautasitishwa  hadi bajaji na boda  boda  kutolewa mjini ,hali  hiyo  imekuwa  tofauti leo baada ya daladala  hizo kuonyesha   kunywea  na kulazimika  kusitisha  mgomo  wenyewe bila hata  kulazimishwa  kufanya  hivyo.


kutoka na   mgomo  huo kusitishwa  leo asubuhi  daladala  zote  zimeonekana  zikiendelea na kazi kama  kawaida  huku  bajaji na boda  boda  nazo zikiendelea  kutoa  huduma bila kunyanyasika na mtu yeyote .

Mmoja kati ya madereva  daladala  mjini hapa ambae hakupenda  kutaja jina lake hapa  alisema  kuwa   mgomo  huo haukuwa na hoja za msingi na ndio  sababu ya madereva hao kutofautiana na kulazimika  kurudi kazini.

Kwani alisema  bajaji  zinazopingwa kufanya kazi hiyo ni zile za Mkwawa ambazo hazizidi hata 20  ila kugoma mji mzima hata kwa daladala za maeneo ambayo Bajaji  hazipo ni  kuwanyanyasa  wananchi na ni sawa na kufanya mgomo  bila  kuwa na madai ya msingi.

Hata  hivyo  baadhi ya  wananchi mjini hapa  wanajipanga kutoa fundisho kwa wamiliki wa daladala  ,chama  cha  daladala hizo na madereva  wao  ili  kuwafikisha mahakamani kudai fidia kwa  kitendo chao cha kuwanyanyasa  kwa siku ya jana.

Mkakati  huo wa kuwafikisha mahakamani  watoa  huduma hao na chama  chao upo jikoni na unafanywa  chini kwa chini na wanaharakati wa haki  za  binadam mjini Iringa pamoja na baadhi ya  wananchi ambao wanapinga kitendo cha daladala  kufanya mgomo  bila kuwapa taarifa  watumiaji wa huduma  hiyo.

Wadau hao  wa usafiri  walisema kuwa  suala la mgomo ni  ruksa kwa mtoa huduma  yeyote  ila kabla ya kufanya  hivyo ni lazima  kutoa taarifa  ya  siku  mbili kabla ya  mgomo  ili   wateja  kuweza kujiandaa kuliko  kugoma ghafla  bila  kuwapa taarifa  wateja.

Walisema  hatua ya  jana  kukosa  huduma  hiyo  wao kama  watumiaji wa  huduma  hiyo  walikwema kufanya shughuli zao za kiuchumi na hata  baadhi yao kushindwa  kufika kwa wakati kazini  hivyo lazima chama hicho cha daladala na  wamiliki kulipa fidia kwa  hasara  waliopata jana .

0 Responses to “DALADALA IRINGA ZANYWEA ZASITISHA MGOMO ZENYEWE WANANCHI WATISHIA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI ...... ”

Post a Comment

More to Read