Tuesday, September 9, 2014
KILA SEKUNDE 40 MTU MMOJA HUJIUA DUNIANI,TANZANIA YASHIKA NAFASI YA 8 RAIA WAKE KUJIUA
Do you like this story?
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dk Margaret Chan |
Wakati
imethibitishwa kwamba katika kila sekunde 40 mtu mmoja duniani huamua kukatisha
maisha yake kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika, Tanzania imeelezwa kuwa ya
nane katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa watu wake kujiua.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bukumbi juzi alipotakiwa
kuthibitisha kwa takwimu kuhusiana na utafiti huo wa WHO, sababu za kujiua na
hata mikoa inayoongoza kwa matukio ya aina hiyo nchini, alitaka mwandishi wa
habari hizi kumtumia maswali ili yafanyiwe kazi kuanzia wiki ijayo.
Utafiti uliofanywa na WHO na kutolewa kama Taarifa na Umoja
wa Mataifa juzi, unaonesha kwamba tatizo la kujiua halitiliwi maanani wala
kujadiliwa kutokana na kunyanyapaliwa na kuwepo kwa imani potofu zinazohusishwa
na vifo hivyo.
Katika utafiti uliotolewa wiki tatu baada ya mmoja wa wakali
wa Hollywood Robin Williams kujiua, pia waandishi wa habari wameonywa dhidi ya
kuelezea kinagaubaga vifo hivyo kutokana na hatari ya watu wengine kunakili
tabia na maamuzi hayo kwa jinsi yalivyoelezwa na vyombo vya habari.
WHO, ambayo imesema kwamba kujitwalia maisha binafsi ni
tatizo kubwa la kiafya duniani kwa sasa linalohitaji hatua madhubuti
kuchukuliwa dhidi yake imetoa taarifa hiyo baada ya kufanya uchunguzi katika
nchi 172 duniani.
Imesema katika mwaka 2012 nchi zenye kipato kikubwa
ziliongoza kwa mauaji ya aina hiyo ikiwa na vifo asilimia 12.7 kwa kila watu
100,000 huku nchi za kipato cha chini na kati zikiwa ni asilimia 11.2 kwa kila
watu 100,000.
Lakini kutokana na nchi za kipato cha chini na kati kuwa na
wingi wa watu, wao ndio waliochukua nafasi kubwa ya vifo hivyo, kwani robo tatu
ya matukio kwa wastani yapo katika nchi hizo.
Hata hivyo, nchi za Kusini Mashariki mwa Asia zikiwemo Korea
Kaskazini, India, Indonesia na Nepal ndizo zimefanya theluthi moja ya waliojiua
duniani.
Vifo vya kujiua katika nchi tajiri vinaelezwa kuwa wastani wa
robo ya vifo vinavyotokea duniani kote vya aina hiyo. Aidha utafiti huo
umeonesha kwamba njia kubwa inayotumika karibu duniani kote ni kutumia sumu za
mashambani, kujinyonga, kujipiga risasi na kuruka kutoka katika majengo marefu
tabia ambayo ipo zaidi katika nchi za Asia, hasa maeneo ya miji.
“Kila kifo cha kujiua huleta huzuni. Inakadiriwa kwamba watu
zaidi ya laki nane hufa kwa kujiua. Lakini pia wapo watu wengi wanaojaribu
kujiua kwa namna tofauti,” alisema Mtendaji wa WHO, Dk Margaret Chan
akihitimisha miaka kumi ya utafiti wa tatizo hilo.
Alisema kwamba athari inayopatikana kwa familia, marafiki na
jamii ni kubwa hata kama watu hao wanakuwa wamejiua wenyewe. Afya ya akili WHO
wamesema takwimu za watu wanaojiua hazipo sawa kutokana na nchi nyingi kutokuwa
na tabia ya kuweka takwimu hizo.
Kutokana na upungufu huo, walilazimika kufanya kazi ya ziada
ili kuweza kupata wastani wa watu wanaojiua nchi kwa nchi. Wastani wa dunia wa
watu kujiua upo kwa watu 11.4 kwa kila watu 100,000 huku wanaume kama wanawake
kwa idadi sawa wakijaribu kujiua.
Nchi ambazo zinaongoza kwa vifo vya kujiua ni Guyana
(asilimia 44.2 kwa kila watu 100,000), ikifuatiwa na Korea Kaskazini na Korea
Kusini (asilimia 38.5 na 28.9 kwa kila 100,000).
Nchi nyingine ni Sri Lanka (28.8), Lithuania (28.2), Suriname
(27.8), Msumbiji (27.4), Nepal na Tanzania (24.9 kila mmoja), Burundi (23.1),
India (21.1) na Afrika Kusini (19.8). Nchi nyingine ni za Russia na Uganda
(zote zikiwa na wastani wa 19.5), Hungary (19.1), Japan (18.5) na Belarus
(18.3).
Katika nchi zenye kipato kikubwa matatizo ya afya ya akili
kama msongo wa mawazo umeelezwa kusababisha asilimia 90 ya vifo vya kujiua
ukilinganisha na asilimia 60 katika nchi za Asia kama China na India, WHO
imesema.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kwamba ni lengo
ifikapo mwaka 2020 kuhakikisha kwamba wanapunguza wastani wa kujiua kwa
asilimia 10.
Hata hivyo, utafiti umeonesha kuna changamoto kubwa kutokana
na vifo hivyo kutokea katika makundi ambayo yanaonekana kutengwa, wengi wao
wakiwa masikini, wenye matatizo mbalimbali na wanaoishi katika hali ya
kutothaminiwa au kukubalika katika jamii.
Magonjwa ya kuambukiza Utafiti umeonesha kwamba nchi zenye
pato dogo ambazo zinahangaika kuwatimizia wananchi wake mahitaji muhimu
yakiwemo ya afya, kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza wana wakati mgumu wa
kutambua na kuwasaidia watu wanaotaka kujiua.
Dk Chan anaamini kwamba vifo vya aina hii (vya kujiua)
vinaweza kuzuiwa. Ametaka nchi mbalimbali kuendelea na kazi ya kuzuia vifo vya
kujiua na hata nchi ambazo hazina watu wanaojiua zifanye juhudi ya kuhakikisha
kwamba zinazuia kutokea kwa vifo hivyo kwa kuwa wazi kujadiliana na kuweka
katika ajenda.
Hata hivyo wataalamu wamekuwa wakishutumu vyombo vya habari
na vile vya kijamii kwa kuelezea jamii kinagaubaga vifo hivyo hali ambayo
inaweza kutumiwa na watu wengine kujiua.
“Kuna kutowajibika kwa vyombo vya habari katika suala hili,
wanaandika tu, wanakuwa chachu, habari zao huchochea vifo zaidi,” inasema
taarifa hiyo huku ikisisitiza kwamba namna zinavyoandikwa ni kama vile kuremba
aina hiyo ya kufa na kuiona kwamba ni hali ya kawaida.
Akizungumzia utafiti huo katika mahojiano na gazeti hili,
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema ni jukumu
la wizara yake kuhakikisha amani katika familia inadumishwa.
Alisema kujiua ni kosa la jinai na pia ni dhambi, hivyo
wizara yake inahamasisha upendo ndani ya familia kuwepo na mazungumzo ili kuepuka
matatizo yanayosababisha watu kujiua.
“Jamii itambue ni vizuri kuongea ndani ya familia tangu watu
wakiwa wadogo ili inapoonekana dalili ya tatizo lipatiwe ufumbuzi na sisi kama
wizara, kazi yetu ni kuhamasisha familia kuishi kwa upendo na mawasiliano ya
mara kwa mara,” alisema Waziri Simba.
via>>Habarileo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ KILA SEKUNDE 40 MTU MMOJA HUJIUA DUNIANI,TANZANIA YASHIKA NAFASI YA 8 RAIA WAKE KUJIUA”
Post a Comment