Saturday, February 28, 2015

IBRAHIM HAJIBU APIGA "HAT TRICK" SIMBA IKIINYONYOA TANZANIA PRISONS MABAO 5-0.




Ligi kuu soka tanzania bara imeendelea kulindima katika viwanja mbalimbali nchini, huku katika dimba la uwanja wa taifa jijini dar es salaam, kukipigwa mtanange wa kukata na shoka kati ya klabu ya wekundu wa msimbazi Simba dhidi ya wajelajela Tanzania Prisons kutoka Jijini Mbeya.

Iliichukuwa Simba takribani dakika 21 kuweza kuandika bao la kwanza kupitia kwa Ibrahim Ajibu baada ya kazi nzuri iliyofanywa na mchezaji raia wa kiganda Emmanuel Okwi, Simba iliendeleza mashambulizi katika lango la Prisons na kumfanya Ibrahim Ajibu kwa mara nyingine tena kupachika bao la pili katika dakika ya 34 ya mchezo.

Nyota ya mchezaji huyo chipukizi iliendelea kung'ara katika mchezo huo kwa kuandika bao la tatu na kufunga "hat trick" kwa mkwaju wa Penati katika dakika ya 41 ya mchezo baada ya mchezaji wa Tanzania Prisons kuunawa mpira katika eneo la hatari, na kuifanya Simba kwenda mapunziko wakiwa kifua mbele kwa mabao matatu kwa bila.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote mbili kushambuliana kwa kasi,lakini Simba ilionyesha kuwa imepania kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwa kuliandama lango la Tanzania Prisons kwa kasi zaidi na kumsababisha mchezaji wa Prisons Nurdin Chona kukubali lawama alipoonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Ramadhan Singano "Messi".

Emmanuel Arnold okwi aliwaamsha mashabiki wa Simba katika dakika ya 74 ya mchezo baada ya kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Prisons na kuiandikia Simba bao la nne, na dakika sita baadae Ramadhani Singano akaitimisha kalamu ya magoli kwa Wekundu wa msimbazi baada ya kufunga bao la tano akipokea pasi safi kabisa kutoka kwake Emmanuel Okwi.

MATOKEO MENGINE

Mbeya City   1   Ruvu Shooting 1

Mgambo JKT 0   Coastal Union 1

Stand United 1  Kagera Sugar  0


0 Responses to “ IBRAHIM HAJIBU APIGA "HAT TRICK" SIMBA IKIINYONYOA TANZANIA PRISONS MABAO 5-0.”

Post a Comment

More to Read