Monday, February 23, 2015

JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT) WATOA KAULI KUHUSU WAHITIMU WAO KUANDAMANA




JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana waliomaliza katika jeshi hilo, kutambua kuwa walikula kiapo cha utii wakati wa kuhitimu mafunzo, hivyo suala la kuandamana ni kinyume na kiapo chao.

Vijana hao waliotumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na kumaliza mkataba wa miaka miwili, wameambiwa shinikizo lao la kulazimisha ajira kwa kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makao Makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, ilisema kipengele kimoja cha masharti ya kujiunga na JKT kinasema baada ya mkataba, wanapaswa kurejea nyumbani na hawapaswi kudai jeshi liwatafutie ajira. Ilieleza kwamba masharti ya jeshi hilo, huwekwa bayana kwa vijana wanapojiunga na JKT.

Vijana hao wanatakiwa kujua masharti hayo na taratibu za JKT na kuelewa kuwa JKT halitoi ajira. Taarifa hiyo ilinukuu kipengele kimojawapo cha masharti, kinachosema “Kwa kipindi chote nitakachokuwa ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba nitarejea nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie ajira/ kazi”.

Ufafanuzi huo ulitolewa, kutokana na vijana zaidi ya 200 waliohitimu mafunzo ya JKT kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2013, kutangaza wiki iliyopita kuwa wataandamana siku yoyote wiki hii kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, kumweleza shida zao, ikiwemo kutokuwa na ajira tangu wamalize mafunzo.

Jeshi hilo lilisema ni vema vijana hao, wakatambua kuwa tatizo la ajira siyo kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima Tanzania, ikiwemo hivyo wanashauriwa kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe.

“Kutokana na dhumuni la kuundwa JKT Taifa, halina dhamana ya kuajiri bali kufunza vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada ya hapo wawe wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi,” ilisema taarifa hiyo.

Hata hivyo, jeshi hilo limesema tangu mwaka 2003 hadi 2014, vijana 24,708 wameajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya hao, vijana 21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670, wameajiriwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kwa upande wa Polisi, vijana 3,965 wameajiriwa ambao kati yao, wavulana ni 2,943, Magereza wameajiriwa 2,139 kati yao wavulana ni 2,044, Zimamoto vijana 100 wavulana wakiwa 78 na taasisi zingine wameajiriwa vijana 592.

Aidha, vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama vile migodi ya dhahabu ya Geita, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Taarifa hiyo ilisema JKT ilianzishwa Julai 10, 1963 kwa lengo la kuwaweka pamoja vijana na kuwapa malezi, kuhusu uzalendo na umoja ili kuondoa dalili za matabaka, zilizoanza kujitokeza katika jamii baada ya uhuru.

Serikali ilirejesha mafunzo ya jeshi hilo kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001 baada ya kusitishwa mwaka 1994.

0 Responses to “JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT) WATOA KAULI KUHUSU WAHITIMU WAO KUANDAMANA ”

Post a Comment

More to Read