Monday, February 23, 2015

NJOMBE IWE MFANO BORA WA DAFTARI LA WAPIGAKURA.




LEO Tanzania inaanza kutekeleza hatua muhimu ya kutimiza matukio mazito, yanayosubiriwa kwa hamu mwaka huu na Watanzania nchi nzima ya upigaji kura ya maoni katika Katiba Pendekezwa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Hatua hiyo muhimu ni kuanza rasmi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kupitia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration (BVR), ambao unaanza leo mkoani Njombe.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilishaufanyia majaribio mfumo huo katika baadhi ya maeneo ndani ya mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Morogoro na mkoani Katavi.

Kwa mujibu wa taarifa ya tume, pamoja na changamoto chache zilizobainika, katika maeneo hayo tume ilifanikiwa kwa asilimia kubwa na ina uhakika mfumo huo utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika daftari hilo bila matatizo.

Tume hiyo ilitaja changamoto chache zilizojitokeza katika majaribio hayo kuwa ni mfumo mzima wa BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na programu zinazotumiwa na mfumo huo na maeneo ya uendeshaji uandikishaji huo.

Tume hiyo imewahakikishia Watanzania kuwa changamoto zote hizo, zimefanyiwa kazi kwa kurekebishwa, ambapo pia BVR zitakazotumika mkoani Njombe, nazo zimefanyiwa marekebisho kutokana na changamoto zilizojitokeza.

Kutokana na maandalizi hayo ni wazi kuwa sasa utaratibu mzima wa watu kujiandikisha katika daftari la kudumu, unaanza rasmi mkoani Njombe.

Hivyo, ni vyema wakazi hao wakajitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kujiandikisha ili waweze kushiriki vyema katika matukio mawili makubwa ya uchaguzi.

Hapa nchini katika chaguzi nyingi zilizopita, ilizoeleka kuona idadi ndogo ya watu wenye umri wa kupiga kura kujitokeza kupiga kura, jambo linalosababisha hata ushiriki katika uchaguzi na wale wanaojitokeza kupiga kura pia uwe mdogo.

Ikumbukwe kuwa kila mtu aliyetimiza miaka 18 ana haki ya kujiandikisha katika daftari hilo na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa kura ya maoni kupigia kura Katiba Pendekezwa na pia kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kuchagua viongozi watakaoliongoza taifa.

Hivyo basi ni vyema wakazi wa Njombe, wakawa mfano mzuri kwa watanzania wa mikoa mingine inayosubiri utaratibu huo wa kujiandikisha, kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili ratiba ya uandikishaji itakavyosogea katika mikoa mingine, watu wawe na mwamko wa kushiriki kikamilifu.

Wapo baadhi ya watu kazi yao ni kulalamika, kunyoosha vidole na kuishia kufanya vurugu matukio muhimu kama hayo yanapojitokeza.

Watu kama hao badala ya kujitokeza na kushiriki, hutafuta visingizio na baadaye wanapokosa fursa ya kushiriki katika uchaguzi huwa wa kwanza kuanzisha vurugu. Tutambue kuwa kila Mtanzania ana haki ya kupiga kura pale atakapofikisha umri wa miaka 18.

Ikumbukwe pia kuwa mtu hawezi kushiriki katika uchaguzi huo na kumchagua kiongozi anayemtaka, kama hatajiandikisha katika daftari hilo la wapiga kura.

Hivyo basi, wakazi wa Njombe watambue kuwa macho na masikio ya watanzania wote kuanzia leo yapo mkoani humo, wakifuatilia kwa kina utaratibu mzima wa kujiandikisha katika daftari hilo, hasa kupitia mfumo huo wa BVR, ambao umezua gumzo nchini tangu utambulishwe na NEC.

Kutokana na ukweli huo, ni wajibu kwa wakazi wa Njombe kushiriki kikamilifu katika shughuli hiyo.

Pia, tume yenyewe ni lazima ihakikishe kuwa ahadi iliyotoa kwa watanzania, kupitia matokeo ya majaribio ya uandikishaji wananchi kupitia mfumo huo wa BVR, inatekelezeka na uandikishaji huo mkoani Njombe unafanyika kwa mafanikio.

0 Responses to “NJOMBE IWE MFANO BORA WA DAFTARI LA WAPIGAKURA.”

Post a Comment

More to Read