Monday, February 9, 2015
MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2014 (FORM FOUR) YAKAMILIKA.
Do you like this story?
Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta) limesema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha nne
uliofanyika Novemba mwaka jana, umekamilika.
Katibu mtendaji wa
Necta, Dk Charles Msonde amesema kuwa “usahihishaji
umekamilika na baraza lipo katika uchambuzi wa kuyapanga na tutakapokamilisha
tutayatangaza”.
Alipoulizwa ni lini
hasa matokeo hayo yatatangazwa, Dk Msonde alisema: “Tumemaliza kusahihisha na mchakato wa kuyapanga ukikamilika
tutawaeleza hivyo msiwe na shaka.”
Katika kipindi cha
miaka miwili mfululizo, mwaka 2012 na 2013, Necta ilitangaza matokeo ya kidato
cha nne mwishoni mwa Februari na mwanzoni mwa Machi.
Matokeo ya Mtihani wa
Kidato cha Nne uliofanyika mwaka 2013 yalitangazwa Februari 22, mwaka jana na
2012 yalizua gumzo kutokana na asilimia 60 ya watahiniwa kufeli.
Kwa kawaida, muhula
wa masomo kwa kidato cha tano huanza Julai, huku Machi na Aprili mchakato wa
kuwapangia shule hufanyika wakati Mei na Juni hutumiwa kwa maandalizi kwa
wanafunzi hao.
Katika matokeo ya
2013 kama ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka 2012, shule binafsi zilikuwa na
matokeo mazuri kulinganisha na za Serikali zilizokuwa zikitamba miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa Necta,
matokeo ya mwaka 2013, shule kongwe za Serikali na zile za vipaji maalumu,
zilishindwa kuingia kwenye orodha ya shule 30 bora.
Shule kongwe
kihistoria zimekuwa zikitoka kapa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa. Tofauti
na matarajio ya wengi, shule hizo nyingi hazikuwamo hata katika orodha ya shule
100 bora.
Baadhi ya shule hizo
ni Fidel Castro ambayo ilishika nafasi ya 83, Malangali (172), Ifunda Ufundi
(205), Jangwani (226), Bwiru (242), Songea Wavulana (257), Pugu (325) na Azania
(333).
Ikiwa ni mwaka mmoja
umekamilika tangu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulipoanzishwa, taasisi
ya Hakielimu ilitoa matokeo ya utafiti wake yanayoonyesha hakuna
kilichofanyika.
Kaimu Mkurugenzi wa
HakiElimu, Godfrey Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha kuongezeka
ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha ya ufaulu huu
kuonyesha kupanda ghafla, kuna changamoto nyingi katika sekta hiyo ambazo bado
hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.
“Mfano
migogoro ya mara kwa mara kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu, ukosefu wa
maabara, vifaa vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo katika gharama za
utoaji elimu nchini kati ya shule za serikali na shule za binafsi,” alisema Boniventura.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2014 (FORM FOUR) YAKAMILIKA.”
Post a Comment