Tuesday, February 17, 2015

RAIS KIKWETE ASHIRIKI MAZISHI YA CHIFU WA WAHEHE ABDUL SAPI MKWAWA, ASHUHUDIA CHIFU MTOTO AKISIMIKWA




Hapa wakat akikabidhiwa dhana na kusimikwa rasmi kuwa chifu

Baadhi ya waombolezaji

Chifu mpya wa wahehe katika picha ya pamoja na Mzee Joseph Mungai na mdogo wa marehemu Saleh Sapi atakayeekaimu nafasi hiyo mpaka kijana huyo atakapofikisha miaka 20




RAIS Jakaya Kikwete jana ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Chifu wa Wahehe Abdul Sapi Mkwawa, 66, yaliyokwenda sambamba na halfa ya kumsimika mwanae wa miaka 13, Adam Abdul Sapi, mwanafunzi wa darasa la saba kuwa chifu mpya wa kabila hilo.


Mazishi ya kiongozi wa kabila hilo la watu wa mkoa wa Iringa aliyefariki Februari 14, mwaka huu yalifanyika katika kijiji cha Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa ndani ya makumbusho yaliyowekwa  fuvu la babu yake, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa.


Mbali na Rais Kikwete wengine waliohudhuria mazishi hayo yaliyofanyika kwa takribani masaa mawili na nusu (kuanzia saa saba mchana hadi saa tisa na nusu) ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Taifa, Phillip Mangulla , wakuu wa mikoa ya Iringa na Mbeya na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, ndugu jamaa na marafiki.


Kabla ya kifo chake, Abdul Sapi Mkwawa aliyekuwa mtoto wa tatu wa Spika wa kwanza mweusi wa bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Adam Sapi Mkwawa alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha maji Afrika cha Kidamali Iringa. Amewahi pia kufanya kazi katika Chama cha Wazalishaji Tumbaku Iringa na Elimu supplies

Alizaliwa Mei 4, 1949 katika kijiji cha Kalenga na kupata elimu ya msingi katika shule za Kalenga na Tosamaganga kati ya mwaka 1956 na 1963.

Mkwaka 1964 hadi 1970 alijiunga na shule ya sekondari Iyunga na Mkwawa ambako alipata elimu ya kawaida na ya juu ya sekondari kabla ya kujiunga na elimu ya juu ya biashara na utawala 1971 hadi 1973.

Mmmoja wa ndugu wa marehemu, Hussein Sapi alisema, mpaka umauti unamkuta, Abdul Sapi Mkwawa alikuwa mtwa (chifu) aliosimikwa mwaka 1999 baada ya kifo cha baba yake Adam Sapi Mkwawa aliyefariki Juni 25, 1999.



Kabla ya maziko ya Chifu huyo, wazee wa kabila la wahehe walimsimika Adam Abdul Sapi ambaye ni mtoto wake wa tano kuwa chifu mpya wa kabila hilo.

Hata hivyo mtoto huyo anayesoma katika shule ya msingi ya Highlands ya mjini Iringa atalazimika kusubiri kuzifanya shughuli za kichifu mpaka pale atakapotimiza miaka 20.

Tangazo lililotolewa mbele ya Rais na ndugu wa karibu wa familia hiyo, Joseph Mungai limesema mdogo wa marehemu Saleh Sapi Mkwawa atashikilia wadhifa huo mpaka pale mtoto huyo atakapofikisha umri huo.

Baada ya mazishi hayo, Rais Kikwete na msafara wake walipata fursa ya kuzungumza na familia ya marehemu nyumbani kwa familia ya marehemu kijijini hapo katika tukio ambalo watu wengine wakiwemo wanahabari hawakuruhusiwa kuingia.

0 Responses to “RAIS KIKWETE ASHIRIKI MAZISHI YA CHIFU WA WAHEHE ABDUL SAPI MKWAWA, ASHUHUDIA CHIFU MTOTO AKISIMIKWA”

Post a Comment

More to Read