Wednesday, June 24, 2015
AFUKUZWA NA WAUGUZI, AJIFUNGULIA BAFUNI.
Do you like this story?
MJAMZITO aliyefahamika kwa jina la Rotha
Bujiku, amejifungulia bafuni karibu na zahanati ya kijiji baada ya kudaiwa
kufukuzwa na wauguzi waliokuwa zamu siku hiyo, kwa maelezo kuwa anajifungua
kila mwaka.
Tukio hilo lilitokea wilaya ya Maswa katika
mkoa wa Simiyu majira ya saa 2 asubuhi baada ya mjamzito huyo kufika katika
zahanati hiyo kwa lengo la kupata huduma ya kujifungulia kwa wataalamu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo
lililovuta umati wa watu, mjamzito huyo alikataliwa kupokewa na muuguzi wa zamu
aliyetajwa kwa jina la Constansia John.
Ilielezwa kuwa muuguzi huyo alikataa kumpokea
kwa madai kuwa mjamzito huyo alishapewa maelekezo tangu awali kuwa anatakiwa
akajifungue katika hospitali ya wilaya ya Maswa kwani amekuwa akizaa watoto kwa
mfululizo.
Inaelezwa kwamba, wakati Rotha akiugulia
maumivu ya uchungu, muuguzi huyo alimpigia simu ya mkononi Muuguzi Mkunga wa
zahanati hiyo, Leticia Kachumi kumjulisha hali hiyo na alipofika alitaka
mjamzito huyo aondoke katika eneo hilo na atafute usafiri ili aweze kufika
katika hospitali ya wilaya kama alivyoelekezwa katika siku za nyuma.
“Leticia alipofika hapo zahanati baada ya
kupigiwa simu na Constansia, licha ya kumuona anaendelea kulalamika kutokana na
uchungu alimwamuru aondoke eneo hilo mara moja na atafute usafiri wa kumfikisha
hospitali ya wilaya iliyoko umbali wa kilomita 36, kwani walishamweleza kuwa
amekuwa akizaa mfululizo na hiyo ni mimba ya kumi na moja,” alisema shuhuda,
Kundi Mageni. (Dk)
Kutokana na hali hiyo, mjamzito huyo
alilazimika kuondoka zahanati hapo bila msaada wowote na baada kufika karibu na
nyumba iliyoko na zahanati hiyo, alikwenda katika bafu la nyumba ya jirani
ambalo halina sakafu na kujifungulia humo na baadaye kusaidiwa na wasamaria
wema waliosikia sauti ya mtoto.
“Kwa kweli huyu mama amejifungulia katika
mazingira machafu na hatarishi kwa afya yake na mtoto aliyemzaa. Kwa kweli hili
ni tukio la kusikitisha. Huwezi kuamini wauuguzi hao ambao ni wanawake
kumtendea mwenzao ukatili wa kiasi hiki,” alisema Pili Kidesela, Diwani wa kata
ya Shishiyu (CCM).
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Jonathan
Budenu aliyefika katika eneo la tukio muda mfupi baada ya kupata taarifa hizo,
alisema kitendo kilichofanywa na wauguzi hao ni kinyume cha maadili ya kazi yao
na hivyo ni lazima hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa wote waliohusika.
Mwingine ajifungulia kichakani Wakati hayo
yakitokea Maswa, mkoani Arusha binti mwenye umri wa miaka 17 alijikuta
akijifungulia kichakani baada ya kuzidiwa uchungu wakati akisubiri kuombewa
kwenye mkutano wa dini uliofanyika Viwanja vya Magereza, Kisongo nje kidogo na
Jiji la Arusha.
Anna Ngitoria, mkazi wa Endurimeti, wilayani
Arumeru, alikuwa miongoni mwa mamia ya wakazi wa Arusha, Kilimanjaro na
vitongoji vyake waliokuwa wamekusanyika kwa wingi kwenye uwanja huo wa magereza
kwa ajili ya kile kilichodaiwa kuwa ni maombi yaliyoandaliwa na kituo kimoja
cha redio cha jijini Arusha, Radio Safina.
Kwa kawaida uongozi wa kituo hicho huandaa
makongamano ya kila mwezi kwenye uwanja huo wa Kisongo na kujumuisha mamia ya
watu, wengi wao wakiwa ni wanawake na wasichana ambao hupendelea kuhudhuria
maombezi hayo kwa matarajio tofauti.
Mikusanyiko ya maombi ya ‘Radio Safina’
imekuwa ikikusanya watu wengi mithili ya ‘Kikombe cha Babu,’ ambacho nacho
kilivuma sana miaka mitatu iliyopita na tukio la msichana huyo kujifungua
katika moja ya matukio hayo kimezua hisia tofauti mjini hapa.
Akizungumza katika hospitali ya Mount Meru
ambapo amelazwa kwa sasa, binti huyo, Anna amekiri kuwa alijifungua kabla ya
wakati kwa sababu alikuwa na ujauzito wa miezi saba tu.
Mtoto wake njiti sasa anahudumiwa katika wodi
maalumu iliyopo hospitalini hapo na wauguzi wanasema anaendelea vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ AFUKUZWA NA WAUGUZI, AJIFUNGULIA BAFUNI.”
Post a Comment