Thursday, June 25, 2015
KIKWETE ASHANGAA WANAOKOSOA KUKOPA
Do you like this story?
RAIS
Jakaya Kikwete amewashangaa wanasiasa wanaokosoa kitendo cha Serikali yake
kukopa fedha nje ya nchi kuwa kinazidisha deni la taifa, kwamba hawana ufahamu
na kufafanua kuwa katika kuharakisha maendeleo ya nchi, kukopa ni jambo la
kawaida.
Alisema
hata mataifa makubwa yaliyopiga hatua kubwa kwenye maendeleo yamekuwa yanakopa
na akasisitiza kuwa uamuzi wa serikali kwenda nje kukopa amekuwa anaufanya ili
kupata fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ambayo itaifanya nchi ipige hatua
kubwa kimaendeleo.
Alitoa
mfano kuwa hata kama mtu anaendesha duka ni lazima akakope benki kama anataka
kuendeleza duka lake, kama hatafanya hivyo kwa kuamini kuwa fedha anazopata kwa
kuuza bidhaa zitalitunisha duka hilo basi asubiri miujiza ya kumpatia faida.
Aliyasema
hayo wakati akizungumzia uamuzi wa serikali yake kuwenda kukopa nje kwa ajili
ya kujenga miundombinu mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa mkongo wa taifa ambao
alisema lengo lake ni kuweka misingi ya miundombinu wakati taifa linapoelekea
kwenye utekelezaji wa ujenzi wa viwanda vya kisasa.
Rais
Kikwete alisema baada ya kufanya uamuzi huo aliamua pia kuwekeza kwenye utafiti
kwa kuhakikisha kuwa Serikal inatenga fedha kwa ajili ya kuwasomesha watafiti,
kununua vifaa vya utafiti na kukarabati vituo vya utafiti ambayo alisema vingi
vilikuwa kwenye hali mbaya.
“Tulianza
na Sh bilioni 10, tunashukuru sasa hivi tupo kwenye Sh bilioni 60 na naamini
kuwa Rais atakayekuja ataendeleze juhudi hizi kwa kutenga fedha zaidi kwa ajili
ya tafiti maana nikiangalia hali ya baadaye ya maendeleo ya nchi hii inategemea
watafiti, wanasayansi na wabunifu,” alisema Rais Kikwete.
Rais
alisema anajivuna kwamba anaondoka madarakani wakati shughuli za utafiti
zimepata uhai na kwamba juhudi zilizofanywa na Serikali yake za kuwaendeleza
wabunifu zimezaa matunda mengi kwani kwa sasa nchi ina watafiti wazee na vijana
wanaofanya mambo makubwa yanayotambulika kimataifa.
Alisema
fedha zilizotolewa na serikali yake zimesaidia kusomesha watafiti 517 katika
kozi za shahada ya uzamili na uzamivu na vituo 20 vimekarabatiwa na miradi 70
ya utafiti imetekelezwa.
“Ndio
maana nasema kiongozi anayekuja asipoliendeleza hili, mwambieni mzee unatuletea
matatizo.”
Mkurugenzi
Mkuu wa Costech, Dk Hassan Mshinda alisema kongamano hilo la nne limewakusanya
wanasayansi, watafiti, watunga sera na wabunifu mbalimbali.
Alisema
mada 80 zitajadiliwa ikiwemo tafiti mbalimbali zilizofanywa na watafiti wa
ndani, kujadiliana changamoto za kupeleka utafiti sokoni na upatikanaji wa
teknolojia na jinsi ya kuhuisha sayansi asili na sayansi ya kisasa.
Dk
Mshinda alimshukuru Rais Kikwete kwa kujali na kuwapa umuhimu watafiti kuliko
miaka ya nyuma na akasema kuwa anaamini kuwa msingi uliowekwa utaendelezwa na
awamu ijayo.
Alisema
juhudi zilzofanyuwa na Rais Kikwete zimeungwa mkono na nchi za Sweden na
Finland ambao nao sasa wameamua kutoa fedha kusaidia juhudi za serikali katika
kufanya tafiti.
CHANZO:HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ KIKWETE ASHANGAA WANAOKOSOA KUKOPA ”
Post a Comment